MADIWANI WACHACHAMAA

BARAZA la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara limekataa kujadili na kupitisha sheria ndogo za ushuru wa leseni wa halmashauri hiyo kwa madai rasmu yake imechelewa kuwafikia.

Katika kikao kilichoketi jana (leo) mjini Tandahimba, madiwani hao walisema hawako tayari kujadili na kupitisha rasmu hiyo ya sheria kwa madai mbali ya kutowafikia kwa wakati, hawajaelimishwa vyakutosha kuweza kuitetea mbele ya wananchi.

Hoja hiyo iliibuka mara baada ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Abdallah Njovu kuwasilisha ombi la kutaka kuongeza ajenda za kikao cha baraza hilo ili kupitisha sheria ndogo za ukusanyaji wa ushuru wa leseni.

Njovu alilazimika mara kadhaa kutoa ufafanuzi juu ya umuhimu wa ajenda hiyo ili kushawishi madiwani kuridhia, hata hivyo alikumbana na pingamizi.

“Waheshimiwa madiwani, sheria hizi zinahitajika haraka ili ziweze kutumika kukusanya mapato kuanzia Januari, Mosi 2012 … tusipopitisha leo basi tuwe tayari kuruhusu halmashauri yetu isikusanye mapato yake” alisema Njovu

Ufafanuzi wa mkurugenzi huyo haukuweza kubadilisha msimamo wa madiwani hao wa kupinga kuongezwa kwa ajenda hiyo ili baraza liweze kupitisha sheria ndogo hizo.

“Suala hili ni nyeti hatuwezi kukubali liingie katika ajenda za kikao hiki, tunahitaji muda kujadili, wananchi wetu wana makato mwengi sana hatuwezi kukurupuka kupitisha hili” alisema Rashidi Namwatika diwani wa kata ya Mnyawa

Alisema “Hata katika vikao vyetu vya ndani tumeshindwa kulielewa, tunaomba kiitishwe kikao kingine kupitisha hili, lakini sio kwa leo”

Kwa upande wake diwani wa kata ya Ngunja Ismail Chipoka alisema pamoja na umuhimu wa suala hilo , mchakato wake haujakamilika kutokana na kuwapo kwa baadhi ya kata ambazo hazijapokea rasmi ya sheria hizo.

“Kata yangu ni miongoni mwa kata ambazo rasmu ya sheria ndogo hazijaletwa, sasa leo hii tunaambiwa tuingize kwenye ajenda ili tupitishe, kwangu naona sio sahihi”

Kwa upande wake Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Menase Ndorome alionesha kusikitishwa kwake na taarifa za kuwapo kwa kata ambazo hazijapata rasmu ya sheria hizo.

“Oktoba 13, mwaka huu rasmu hizo zilisambazwa katika kila kata, kama kuna kata hazijapata hilo ni suala lingine, tuliwakabidhi watendaji wa vijiji, tutafuatilia na wale watakaobainika kuwa kikwazo tutawachukulia hatua za kinidhamu” alisema Ndorome

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Ali Ndingo alimsihi mkurugenzi kukubaliana na hoja za madiwani za kutaka kutoingizwa kwa ajenda hiyo kutokana na umuhimu wake.

“Naomba hili tuliache, ila madiwani tuwe tayari kuja kupitisha hili hata kama hakutakuwa na posho, tukubali kujitolea kwa nia njema” alisema Ndingo

Kufuatia hoja hizo Njovu aliridhia kuondoa kwa ajenda hiyo hata hivyo haikuelezwa kikao cha kupitisha sheria hizo ndogo za halmashauri kitakutana lini.

Mwisho

Advertisements