SERIKALI YAZIDIWA KETE- KANGOMBA YATAWALA TANDAHIMBA’

UNUNUZI wa korosho kupitia mfumo usio rasmi unaojulikana kwa jina la ‘Kangomba’ umeelezwa kushamiri katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.

Hatua hiyo imeripotiwa wakati serikali kupitia bodi ya korosho imetangaza vita dhidi ya watu wanaojihusisha na ununuzi wa korosho kinyume cha sheria kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao .

Kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tandahimba, Abdallah Njovu ununuzi wa korosho kupitia kangomba umeshamiri katika baadhi ya maeneo wilayani humo hivyo ametoa wito kwa wananchi kushirikiana katika kudhibiti hali hiyo.

Akitoa taarifa ya hali ya ununuzi wa zao la korosho wilayani humo katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi jana (leo) mjini Tandahimba, Njovu alisema kufuatia hali hiyo halmashauri imewakumbusha watendaji wa vijiji kuhakikisha korosho zote zinasafirishwa kwa mujibu wa sheria.

“Nimewaambia watendaji wa vijiji na kata kuhakikisha wanadhibiti kangomba, pia wananchi watakaowezesha kukamatwa kwa watu wanaosafirisha korosho kupitia njia zisizo halali watazawadiwa” alisema Njovu bila kutaja aina ya zawadi.

Alibainisha kuwa katika kudhibiti mianya ya ukiukwaji wa ununuzi wa korosho kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani, pia serikali imevifutia leseni ya ukusanyaji korosho vyama vya wakulima ambavyo sio vyama vya msingi vya ushirika wa kilimo na masoko.

“Umoja wa Wakulima wa Korosho Tandahimba (Uwakota) ni miongoni mwa vyama vilivyozuiliwa, msimu uliopita walifanya kosa kubwa sana ambalo tumeamua kuwafungia hadi pale watakapotekeleza matakwa yetu, sio kwa mwaka huu tena” alifafanua mkurugenzi huyo.

Baadhi ya madiwani madiwani walionesha kutokubaliana na hatua za kuifungia Uwakota, hata hivyo walishindwa kutengua maamuzi hayo kutokana na uwamuzi huo kubarikiwa na ngazi za juu za serikali.

“Sote tunafahamu kuwa Uwakota ni mkombozi wa wakulima Tandahimba, iweje leo wafungiwe? kama suala ni tuhuma za kujihusisha na ununuzi wa kangomba mbona leo hii Uwakota hawafanyi kazi na watu wananunua kangomba” alihoji Makuyeka Makuyeka diwani wa kata ya Chikongola.

Mwisho

Advertisements