KADA WA CCM; SERIKALI YA KIKWETE INAWEKA REHANI AMANI

Abdallah Bakari,
Mtwara
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Makaburi Phiri (77) amesema serikali imeweka rehani amani ambayo kwa sasa Tanzania inajivunia, kwa kuruhusu ongezeko la pengo baina ya matajiri na masikini.
Phiri ambaye aliwahi kuwa katibu wa TANU wilayana baadaye katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya na Mwalimu Nyerere, alisema hayo jana jioni katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika nyumbani kwake Shangani mjini Mtwara.
Alisema ugumu wa maisha kwa masikini umekuwa ukiongezeka siku hadi siku huku matajiri wachache wakiendelea kunufaika na rasilimali za nchi hali ambayo alisema ni tishio la amani kwa siku zijazo.
“Kizazi cha siku za usoni ni kizazi cha wasomi, ni kizazi ambacho hakitakubali utajiri wa nchi unufaishe wachache, hawatakubali walale njaa wakati mwingine anatupa chakula…hakutakuwa na amani hapo baadaye iwapo hali itaendelea kuwa hivi” alisema Phiri
Aliongeza kuwa “Wasomi wanaongezaka na nafasi za ajira zinapungua, kizazi ambacho ni cha wafanyakazi ndicho kinachoendelea kupata ajira, hii ni hatari, wasomi watajazana mitaani na watakapoamua kudai haki yao, vurugu zitatokea”
Aliongeza kuwa mfumuko wa bei kumesababisha wananchi wengi kuishi maisha ya taabu hali inayochagiza malalamiko mengi kwa serikali yao.
“Shilingi 200 tulikuwa tunakula chakula, leo hii labda chai ya mkono mmoja…watu hawawezi tena kula milo mitatu, kila kitu kipo juu, unafiriki nini hatma yake kama si kuvunjika kwa amani” alihoji kada huyo ambaye pia aliwahi kuwa mkuu wa wilaya katika serikali ya awamu ya kwanza na pili.
Akizungumzia utawala wa hayati Mwalimu Nyerere, Phiri alisema Mwalimu alifanikiwa kujenga usawa baina ya matajiri na masikini kinyume na serikali zilizofuata.
“Katika serikali hizi tatu yaani ya Mwinyi, Mkapa na Kikwete, serikali ambayo kwa kiasi fulani ilifuata misingi ya Mwalimu ni serikali ya Mkapa isipokuwa alitofautiana na sera yake ya ubinafsishaji kwa kweli hili alikosea” alibainisha
Huku akionesha kuguswa na utawala wa Mkapa alisema “Mkapa aliweza kupunguza pengo baina ya matajiri na masikini, bidhaa zote muhimu zilikuwa bei chini, kama chai wote tulikuwa tunakunywa si hali ya leo”
Phiri alishauri serikali kubadili mfumo wa elimu na kujenga mfumo mpya ambao utawawezesha wahitimu kujiajiri ili kukabiliana na tishio la ukosefu wa amani linalosababishwa na ukosefu wa ajira
“Tuwe na mfumo wa elimu utakaowajengea uwezo wahitimu kujiajiri katika ujasiliamali, elimu ya sasa inatengeneza matabaka baina ya wenye nacho na masikini ambayo ni hatari kwetu”
Mwisho

Advertisements