MTWARA WALALAMIKIA UGUMU WA MAISHA

Abdallah Bakari,
Mtwara
WAKAZI wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani wameiomba serikali kuchukua hatua za makusudi na za haraka kukabiliana na ugumu wa maisha unaowakabili ambao unaosababishwa na mfumuko wa bei kwa bidhaa muhimu.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti jana, wananchi hao walisema gharama za maisha zimepanda katika kiwango ambacho huwalazimu kupunguza idadi ya milo kutoka mitatu na kufikia miwili na wengine mmoja.
Walibainisha kuwa bei ya vyakula imepanda wakati hali ya kipato ikizidi kushuka chini kitendo kinachosababisha wakabiliwe na ugumu katika kuyapata mahitaji muhimu ya binadamu hususani chakula.
“Leo hii mchele kilo moja sh. 2,000 unga wa mahindi sh. 1,200, sukari 2,500, wakati pato letu ni chini ya sh. 1,000 kwa siku, unafikiri nini kitatokea kama si kupunguza idadi ya milo” alisema Shufaa Mwidini (31) mkazi wa mjini hapa
Alifafanua kuwa “Mwezi mmoja uliopita mchele ulikuwa sh. 1200, unga wa mahindi sh.800 wakati sukari ilikuwa sh. 1800 … bei hizo tuliweza kumudu kwa baadhi yetu lakini kwa sasa hali ni ngumu, nakula milo miwili tu, asubuhi na usiku, naomba serikali ichukue hatua za makusudi kukabiliana na hali hii”
Mkazi mwingine wa magomeni mjini hapa, Jauma Saleh (41) alisema serikali ina wajibu wa kuhakikisha maisha yanakuwa rahisi kinyume na hali ya sasa ambayo alifananisha na mzazi aliyemtelekeza mwanae.
“Inawezekana viongozi serikalini hawajui ugumu wa maisha tunaopata japo tunanunua bidhaa kwa bei moja, tofauti ni kwamba wao wanafedha kiasi bei hiyo haiwaathiri na sisi hatuna fedha ndiyo maana tunalalamika” alisema Saleh
“Unajua uliyeshiba hamjui mwenye njaa, huwenda hiyo ikawa sababu ya viongozi kuchelea kuchukua hatua, ugumu wa maisha unaotukabili si wa mficho kiasi serikali isubiri iambiwe ili ichukue hatua…nilikuwa napata milo miwili kwa siku sasa napiga ndefu yaani mlo mmoja tu wa mchana” alisisitiza
Jackson Daniel (27) ni mfanyabishara wa vyakula katika soko ndogo la Kiyangu, alisema wanalazimika kupandisha bei vyakula kutokana na kupanda kwa bei ya manunuzi na gharama za usafiri.
“Biashara ni faida, kama hupati faida hiyo si biashara…bei ya manunuzi ya mchele, unga, sukari, mafuta imepanda hivyo ili nasi tupate faida ni lazima tupandishe, usafirishaji nao upo juu hayo yote yanachangia” alisema Daniel
Mwisho

Advertisements