WAKULIMA WA KOROSHO TANDAHIMBA WAMTAKA MAGHEMBE

Abdallah Bakari,
Tandahimba.
WAKULIMA wa korosho wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara wamemtaka Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe kutembelea wilaya hiyo kupata maelezo yo ya kina yatakayomwezesha kuupatia ufumbuzi mgogoro unaofukuta kwa sasa baina ya serikali mkoani huo na wakulima hao.
Oktoba, 16, mwaka huu serikali mkoani hapa imeingia katika mgogoro na wakulima wa korosho baada ya kusitisha shughuli za ukusanyaji wa korosho na kuziuza chini ya mfumo wa stakabadhi ghalani zilizokuwa zinafanywa na vyama vya kijamii vilivyoundwa na wakulima hao.
Kwa mujibu wa serikali, sababu kuu ya kuvizuia vyama hivyo ni kutokana na uzoefu walioupata kwa Umoja wa Wakulima wa Korosho Tandahimba (Uwakota) kuwa msimu uliopita walijihusisha na ununuzi wa korosho kupitia mfumo batili wa kangomba.
Uwakota imekuwa ikisifika kwa kuwakomboa wakulia ambapo msimu ulipita waliwalipa wanachama wao 1880 sh. kwa kilo ya korosho ghafi, bei ambayo haijawahi kufikiwa na vyama vya msingi vya ushirika.
Wakulima hao kwa nyakati tofauti walisema wamepoteza imani na viongozi wa mkoa na kwamba wanaamini haki haiwezi kutendeka iwapo waziri Maghembe atafanyia kazi maelezo ya upande mmoja hivyo walimtaka kuwatembelea.
“Tangu waziri wa kilimo ateuliwe hajawahi kuja huku, sasa kwa kuwa tuna mgogoro na serikali tunamtaka aje kupata maelezo kutoka kwetu sisi wakulima…hatuna imani na serikali ya mkoa katika hili” alisema Shabia Nassoro makazi wa Mdimba
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi mwishoni mwa wiki katika vijiji vya Matogoro, Mwindi, Mdimba, Mambamba, Milongodi na Mkomolela wilayani Tandahimba umebaini kuwa licha ya serikali kuifungia Uwakota, ununuzi wa kangomba umeshamiri wilayani humo.
Mwananchi imeshuhudia wananchi wakiuuza korosho katika vijiji hivyo kwa uwazi mkubwa, huku wakishtumu serikali kuchagiza uuzaji huo na kwamba kitendo cha kuvifungia vyama vya kiraia kinaweza kutafsiriwa kuwa ni uonevu wa serikali dhidi ya wananchi wake.
Katika kijiji cha Matogoro, Abilah Mohamedi alishuhudiwa na mwandishi wa habari hizi akiuza korosho kwa kangomba, huku akiitupia lawama serikali kuwa imekuwa ikichagiza ununuzi huo kwa kushindwa kupeleka fedha kwenye vyama vya msingi kwa wakati.
“Tatizo la kangomba sio Uwakota, tatizo ni serikali yenyewe, leo hii katika vyama vya msingi hakuna fedha na mtu una shida kwa nini basi usiuze kwa kangomba ili umalize shida zako, unajua kimfaacho mtu chake” alisema Mohamedi
Huku akioneshwa kukerwa na uwamuzi wa serikali kuufungia Uwakota alisema “Ni serikali ya ajabu sana, serikali ambayo inataka wananchi wake waendelee kuwa masikini, hakuna aliyefikiria kuwa utendaji mzuri wa Uwakota katika kuwakomboa wakulima mwishowe utakuwa kuufungia badala ya kuupongeza”
Katibu msaidizi wa chama cha ushirika cha Milongodi, Ahamadi Mbene alisema chama chake kwa wiki mbili sasa kimekosa fedha kutokana na kushindwa kuwasiliha stakabadhi ya mazao ghalani benki ili waweze kupatiwa fedha zingine.
“Tunayo tatizo la usafiri, lakini pia ghalani kumejaa hivyo hatuwezi kupeleka mzigo ili tupate stakabadhi ya mazao ghalani…ni wiki mbili sasa hatuna fedha” alisema Mbene
Aidha uchunguzi huo umebaini kuwa licha ya serikali kuituhumu Uwakota kuhusika na ununuzi haramu, vyama vya msingi na baadhi ya serikali za vijiji vimebairiki mfumo huo usio halali.
Diwani wa kata ya Milongodi, Ramadhani Ulaya alisema serikali za vijiji katani humo, vimeruhusu ununuzi wa kangomba kwa sharti la wanunuzi kuuza korosho zao katika vyama vya ushirika vilivyo katika vijiji huska.
“Tunajua kuwa serikali imezuia hili, lakini tumebaini utekelzaji wake ni mgumu, hivyo tumeruhusu ununuzi wa kangomba … watendaji wa vijiji wanawajibu wa kuhakikisha wanunuzi wanauza korosho hizo katika vyama vya msingi vya maeneo yao, atakayeruhusu kutoroshwa, huyo atawajibishwa” alisema Ulaya
Naye mnunuzi Hamisi Athumani aliyekutwa ananunua katika kijiji cha Matogoro alisema kilo moja ya korosho ananunua kwa bei dira ya serikali ya 1200 sh. na kwamba kwa siku anaweza kupata wastani wa kilo 100.
“Mimi ni mdandaji, sio mkulima wala mwanachama wa Uwakota, nikinunua hapa nakwenda kuuza ghalani kwenye chama cha msingi cha ushirika, faida yangu ni pale inapotokea malipo ya tatu” alibainisha.
Mwisho

Advertisements