DIWANI ARUHUSU KANGOMBA

Abdallah Bakari,
Tandahimba.
LICHA ya serikali kupiga marufuku ununuzi wa korosho kupitia mfumo batili wa kangomba, diwani wa kata ya Milongodi, wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, Ramadhani Ulaya ameruhusu ununuzi huo katika kata yake.
Akizungumza na Mwananchi juzi katani humo, Ulaya alisema kamati ya maendeleo ya kata hiyo imefikia uwamuzi wa kupingana na tamko la serikali la kupiga marufuku Kangomba baada ya kubaini utekelezaji wake kuwa mgumu.
Alibainisha kuwa pamoja na kuruhusu ununuzi huo, wafanyabiashara ya kangomba wamewekewa sharti la kuhakikisha wanauza korosho hizo kwenye vyama vya msingi vya ushirika vilivyopo katika vijiji huska.
“Tunajua kuwa serikali imezuia hili, lakini tumebaini utekelzaji wake ni mgumu, hivyo tumeruhusu ununuzi wa kangomba … watendaji wa vijiji wanawajibu wa kuhakikisha wanunuzi wanauza korosho hizo katika vyama vya msingi vya maeneo yao, atakayeruhusu kutoroshwa, huyo atawajibishwa” alisema Ulaya
Aliongeza kuwa “Serikali imetufikisha hapa, leo fedha ghalani hakuna kwa wiki mbili sasa, unaposema watu wasiuze kwa kangomba unataka shida zao watatue kwa fedha kutoka wapi kama si kuuza korosho zao, hivyo tuliona busara sana kuruhusu kangomba katika mazingira haya”
Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania ilipiga marufuku ununuzi wa korosho nje ya mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ujulikano kama kangomba, kwa madi umekuwa ukiwanyonya wakulima wa zao hilo.
Kauli hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa bodi hiyo, Anna Abdallah katika mkutano wa wadau wa zao hilo uliofanyika mjini Llindi Septemba mwaka huu, ambapo mkutano huo ulitangaza bei dira ya korosho kuwa sh. 1200 kwa kilo.
Moja ya hatua zilizochukuliwa na serikali katika kupambana na kangomba ni pamoja na kuufungia Umoja wa Wakulima wa Korosho Tandahimba (Uwakota) kwa madai ulijihusisha na ununuzi wa korosho kwa kangomba katika msimu uliopita.
Mwananchi imeshuhudia wananchi wa vijiji vya Matogoro, Mwindi, Mdimba, Mambamba, Milongodi na Mkomolela wilayani Tandahimba wakiuza korosho kwa uwazi mkubwa, huku wakishtumu serikali kuchagiza uuzaji
Katika kijiji cha Matogoro, Abilah Mohamedi alishuhudiwa na mwandishi wa habari hizi akiuza korosho kwa kangomba, huku akiitupia lawama serikali kuwa imekuwa ikichagiza ununuzi huo kwa kushindwa kupeleka fedha kwenye vyama vya msingi kwa wakati.
“Tatizo ni serikali yenyewe, leo hii katika vyama vya msingi hakuna fedha na mtu una shida kwa nini basi usiuze kwa kangomba ili umalize shida zako, unajua kimfaacho mtu chake” alisema Mohamedi
Katibu msaidizi wa chama cha ushirika cha Milongodi, Ahamadi Mbene alisema chama chake kwa wiki mbili sasa kimekosa fedha kutokana na kushindwa kuwasiliha stakabadhi ya mazao ghalani benki ili waweze kupatiwa fedha zingine.
“Tunayo tatizo la usafiri, lakini pia ghalani kumejaa hivyo hatuwezi kupeleka mzigo ili tupate stakabadhi ya mazao ghalani…ni wiki mbili sasa hatuna fedha” alisema Mbene
Naye mnunuzi Hamisi Athumani aliyekutwa ananunua katika kijiji cha Matogoro alisema kilo moja ya korosho ananunua kwa bei dira ya serikali ya 1200 sh. na kwamba kwa siku anaweza kupata wastani wa kilo 100.
“Mimi ni mdandaji, sio mkulima wala mwanachama wa Uwakota, nikinunua hapa nakwenda kuuza ghalani kwenye chama cha msingi cha ushirika, faida yangu ni pale inapotokea malipo ya tatu” alibainisha.
Mwisho

Advertisements