MKUU WA MKOA ATAKA WABUNGE MTWARA KUTETEA MKOA WAO

MKUU wa mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia, amewataka wabunge wa Mtwara kuungana katika kupigania maendeleo ya mikoa yao, pindi wawapo bungeni.

Rai hiyo ameitoa jana wakati akifunga kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika mjini hapa, ambapo alisema maendeleo ya mikoa hiyo yanategemea zaidi nguvu za kisiasa katika kuishawishi serikali kuwaletea maendeleo wananchi wa maeneo hayo.

“Sisi tunasema kilimo Kwanza, lakini ninyi wabunge muwapo bungeni unganeni na semeni Mtwara kwanza, kuweni kitu kimoja munapopigania maendeleo ya mkoa wetu…huyu akisimama akaongea jambo hilohilo na yule kasisitizia na mwingine akaunga mkono basi ni rahisi kwa serikali kusikiliza kilio chenu” alisema Simbakalia aliyekuwa mwenyekiti wa kikao hicho.

Alitolea mfano wa mkoa wa Kigoma ambapo alisema maendeleo waliyofikia ni matunda wa wabunge wa mkoa huo kuimba wimbo mmoja bungeni katika kuhakikisha serikali inazipatia ufumbuzi kero mbalimbal zilizokuwa zinaukabili mkoa huo.

“Kule Kigoma (Alikokuwa mkuu wa mkoa kabla ya kuhamishiwa Mtwara) tuliwaambia wabunge waseme Kigoma kwanza walifanya hivyo na mambo sasa swari na huku Mtwara hebu fanyeni kama ilivyokuwa kwa wezenu” alisisitiza.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wabunge wa mkoa wa Mtwara, Anna Abdallah aliwakumbusha watendaji kuzingatia thamani ya fedha katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao.

“Kwa sasa tumewaambia ma-auditor (wakaguzi) wasiangalie performance (utekelezaji), mkazo zaidi uwe kukagua value for money (thamani ya fedha),huko ndiko kwenye matatizo…nawaombeni sana utekelezaji wa miradi lazima uendane na fedha zilizotumika” alisema Abdallah

Alisema taarifa zilizotolewa katika kikao hicho zinaonesha kuwapo kwa mafanikio makubwa katika sekta ya barabara hivyo alitumia muda huo kuwasihi watendaji uzuri wa taarifa usiishie katika makaratasi mbali ushabihi hali halisi.

Mwisho