WANAFUNZI 22 MATATANI VURUGU NDANDA

WANAFUNZI 22 MATATANI KWA VURUGU NDANDA

Abdallah Bakari,

Masasi.

WANAFUNZI 22 kati ya 1198 wa shule ya sekondari ya juu ya wavulana Ndanda, wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, wanatarajia kujieleza mbele ya bodi ya shule hiyo kutokana na tuhuma za kushawishi na kuongoza wenzao kufanya vurugu shuleni hapo. 

Wanafunzi hao wanadaiwa kufanya maandamano kwa kutembea kwa mguu umbali wa jumla kilomita 74 kwenda na kurudi mjini Masasi, makao makuu ya wilaya hiyo wakidai kujengewa msikiti shuleni hapo. 

Katika madai yao ya msingi wanafunzi hao wanaomba serikali kujenga msikiti shuleni hapo, ili kuleta uwiano wa kuabudu kutokana na uwepo wa kanisa shuleni hapo. 

Shule hiyo awali ilikuwa inamilikiwa na Kanisa Katoliki ambalo lilijenga kanisa kabla ya serikali kuitwaa. 

Mbali na maandamano hayo yaliyotia nanga ofisi ya mkuu wa wilaya, wanafunzi hao wanadiwa kutoa lugha ya vitisho kwa walimu hali iliyolazimu uongozi wa shule hiyo kuifunga kwa dharura Desemba, 5 mwaka huu ili kuruhusu uchunguzi kubaini chagizo la hali hiyo.

Mkuu wa shule hiyo, Joseph Sowani aliliambia gazeti hili kuwa baada ya uchunguzi huo wanafunzi 22 wamebainika kuongoza ghasia hizo, hivyo watajieleza mbele ya bodi ya shule Desemba, 21 mwaka huu huku wakiwa wameambatana na wazazi wao. 

“Desemba, 7 mwaka huu bodi ya shule iliketi na kukubaliana kuwa wanafunzi 22 waletwe mbele yao wakiwa wameambatana na wazazi wao, kikao hicho kitaketi Desemba 21, mwaka huu” alisema Sowani 

Aliongeza kuwa “Shule itafunguliwa Desemba, 27 mwaka huu, huku wanafunzi na wazazi wakiwa wametumiwa sheria za shule na kukbaliana nazo, kwa kujaza fomu maalum ambazo zinapatikana kwenye tovuti ya shule hiyo (www.ndandaseco.dinstudio.com)” 

Alisisitiza kuwa hakuna mwanafunzi atakayepokelewa shuleni hapo bila kujaza na kusaini fomu za kukubali kutii sheria za shule na kanuni zake. 

MwishoAdvertisements