MBUNGE AKERWA BARABARA KUTENGENEZWA MASIKA

Huu ndiyo usafiri wetu kwenda hospitali Tandahimba

Ujenzi wa barabara masika

MBUNGE wa Tandahimba, mkoani Mtwara, Juma Njwayo ameeleza kutoridhishwa kwake na hatua zinazochukuliwa na Wakala wa Barabra Nchini (Tanroads) mkoani humo, kukarabati barabara za jimbo hilo wakati wa masika kwa madai kuwa hali hiyo inasababisha usumbufu kwa watumiaji.

Mbunge huyo alibainisha hayo katika kikao cha bodi ya barabara kilichofanyika mjini Mtwara jana, ambapo alieleza kuwa barabara hizo kwa sasa zimekuwa zikipitika kwa shida na wakati mwingine kusababisha abiria kulala njiani, kitendo ambacho alieleza wazi kutoridhishwa nacho.

“Kuna jambo la kushangaza kule jimboni kwangu, wakati wa kiangazi barabara hazifanyiwi matengenezo, ila mvua zikianza kunyesha utaona makandarasi wanaanza kukarabati…hali hii husababisha barabara hizo kupitika kwa shida wakati huu wa masika” alisema Njwayo

Aliongeza kuwa “Kwanini basi zisifanyiwe ukarabati wakati wa kiangazi ili masika wananchi wasafiri kwa urahisi zaidi…naomba Tanroad kuliangalia hili katika muundo ambao utawaondolea adha watumiaji wa barabara badala ya hali ya sasa”

Sanjari na hilo mbunge huyo aliiomba wakala hiyo kuhakikisha katika bajeti ijayo mji wa Tandahimba unatengewa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilomita tano za barabara kwa kiwango cha lami, kama ilivyo kwa makao makuu ya wilaya zingine.

“Tunaomba katika bajeti ijayo kuwepo na fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ya kilomita tano katika mji wa Tandahimba, kwetu sisi wanasiasa inatupa shida kueleza mafanikio ya serikali hasa kwenye sekta ya barabara iwapo jimboni kwako hawaijui lami” alisema mbunge huyo

Akijibu hoja hizo, Mhandisi wa Tanroad mkoani hapa, Mussa Mataka alisema hatua ya kukarabati barabara za wilaya ya Tandahimba wakati wa masika inatokana na wilaya hiyo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa maji.

“Makandarasi wanakataa kutengeneza barabara hizo wakati wa kiangazi kutokana na ukosefu wa maji, wanalazimika kwenda umbali wa zaidi kilomita 40 kufuata maji kitendo ambacho ni hasara kwao … tunalifahamu hilo ila kutokana na mazingira inatulazimu tufanye hivyo” alifafanua mhandisi Mataka

Aliongeza kuwa “Hata hivyo tumewasiliana nao ili kuona njia bora za kukarabati barabara wakati huu wa masika bila kuathiri kwa kiwango kikubwa watumiaji wa barabara hizo, tumewaagiza kuimarisha barabara za michepuo wakati wa ujenzi…pia hili la lami Tandahimba, limezingatiwa na tutahakikisha bajeti ijayo inakuwapo”

Mwisho

Advertisements