KIKWETE ADANGANYWA TENA

MARA kadhaa tumesikia wateule wa Rais Jakaya Kikwete wakimuongopea

Rais Jakaya Kikwete

katika taarifa zao mbalimbali, katika tukio la hivi karibuni Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba Newala (Tanecu) ‘kimemdanganya’ rais juu ya ujenzi wa ghala la kuhifadhi mazao linalojengwa na chama hicho mjini Tandahimba.

Uchunguzi wa KUSINI umebaini kuwa katika taarifa ya ujenzi wa ghala hilo iliyosomwa na mwenyekiti wa Tanecu Yusuph Nannila kwa Rais Kikwete, Julai, 27 mwaka huu kulikuwa na udanganyifu juu ya uwezo wa ghala hilo kuhifadhi korosho.

Katika taarifa hiyo, rais alielezwa kuwa ghala hilo lina uwezo wa kuhifadhi tani 10,000, uchunguzi umebaini kuwa taarifa hiyo si ya kweli na kwamba ghala hilo lina umewezo wa kuihifadhi tani 35,00 tu.

“Hili ghala lina uwezo wa kuhifadhi tani 3500 tu, tena hizo ni kwa kuzilazimisha, yaani kinyume na taratibu za uhifadhi…hicho ndicho ninachokifahamu mimi kama mwendesha ghala, kama rais aliambiwa tani 10,000 mimi sijui” alisema mmoja wa maofisa wanaondesha ghala hilo kwa sharti la kutotajwa jina.

Meneja wa Tanecu Daimu Mpakate alikiri ghala hilo kuwa na uwezo mgodo wa kuhifadhi kuliko walioueleza kwa rais alipotembelea na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa ghala hilo Julai mwaka huu.

“Michoro yote inaonesha kuwa ghala litakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 za korosho sasa tunafuatilia kujua tatizo lipo wapi…we mtoto acha umbea hiyo si habari ya kuandika, kuna habari nyingi huku, njoo jionee mwenyewe” alisema Mpakate akiongea kwa simu

Mwenyekiti wa Tanecu, Nannila alisema amewaagiza watendaji wake kufuatilia suala hilo ili kujua undani wake kwa kuwa mkataba wa ujenzi wa ghala hilo ulifanyika na uongozi uliopita hivyo hawezi kuongelea kwa kina.

“Mchakato wa ujenzi wa ghala lile ulianza kabla ya mimi kuingia madarakani, hivyo nimewaagiza watendaji wangu kulifanyia kazi hilo…tulipoandika ile taarifa tulizingatia nyaraka zinasema nini, wakati ule ghala lilikuwa halijaanza kufanya kazi, lilipoanza kufanya kazi ndiyo tumebaini haya” alisema Nannila ambaye anasifika kwa utendaji kazi uliotukuka.

Mwisho

Advertisements