BIASHARA YA KOROSHO YAINGIA ‘MAJI’

 

HALI ya soko la Korosho mkoani Mtwara imeendelea kuwa tete kwa zaidi ya miezi miwili hivi sasa, huku wakulima wakikopesha korosho zao pasipo kufahamu lini watalipwa.

Wakulima na korosho ghalani, wilayani tandahimba, mkoani Mtwara

Habari za uhakika zinasema kuwa zaidi ya tani 40,000 za korosho zipo kwenye maghala yanayotumika kuhifadhi zao hilo chini ya mfumo wa ununuzi wa Stakabadhi ya Mazao ghalani.

Korosho hizo ni mbali na zile ambazo bado zimo mikononi mwa wakulima, huku sababu kuu ikitajwa kuwa ni kuwapo kwa mgomo baridi wa wanunuzi wa zao hilo.

Kutokana na hali hiyo ununuzi wa zao hilo mikononi mwa wakulima umesimama na sasa biashara ya kukopesha ndiyo inayoendelea baina ya wakulima na vyama vya msingi vya ushirika.

Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania ilitangaza bei ya korosho kwa kilo 1200 ambapo mkulima angelipwa asilimia 70 ya bei kabla ya malipo ya pili ambayo yangekuwa asilimia 30, kutokana na hali iliyojitokeza wakulima sasa wanakabidhi korosho kwa vyama vya ushirika bila malipo ya hata senti tano.

Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania, Anna Abdallah anajitetea kwa kusema kuwa hali hiyo inasababishwa na hujuma zinazofanywa na wapinga mfumo wa stakabadhi ghalani hivyo kusababisha mateso bila ya chuki kwa wakulima.

“Kumekuwapo na hujuma kubwa zinazoendelea katika biashara ya korosho, zaidi ya tani 40,000 zipo katika maghala mbalimbali ya kuhifadhi korosho katika mkoa wa Mtwara na Lindi…bado wakulima wetu wanazo korosho nyingi” alisema Abdallah akitoa taarifa ya hali ya ununuzi wa korosho kwa kamati ya ushauri ya maendeleo ya mkoa wa Mtwara  iliyofanyika hivi karibuni.

Mwisho

Advertisements