MEMBE-KUWENI MACHO NA WANASIASA WANAOJIPENDEKEZA

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa bernad membe, mbunge wa Mtama mkoani Lindi

amewataka viongozi wa dini kuwa macho na wanasiasa wanaotumia nyumba za ibada kujisafisha kwa jamii ili kulinda maslahi yao binafsi.

Membe aliyasema hayo mjini Mtwara juzi katika hafla fupi ya kuliombea Taifa iliyoandaliwa na Mbunge wa Mtwara Mjini, Asnein Murji na kuwakutanisha viongozi mbalimbali wa dini za Kiislam na Kikristo nyumbani kwa mbunge huyo.

Alisema amani ya Taifa imo shakani iwapo viongozi wa dini wataruhusu nyumba za ibada kuwa kimbilio la wanasiasa na wao kutumika kuwasafisha kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha mgawanyiko kwa jamii.

Alifafanua kuwa iwapo viongozi wa dini wataruhusu hali hiyo wanaweza kuligawa Taifa kwa kila muumini kumfuata mwanasiasa wa mrengo wake kitendo ambacho alionya kuwa ni hatari

“Viongozi wa dini msipokuwa makini mutaliingiza Taifa katika machafuko…hakuna chama chochote cha siasa kinachoweza kuvuruga amani yetu, ila ninyi viongozi wa dini mkiamua munaweza kuvuruga amani yetu” alisema Membe

Aliongeza kuwa “Kuweni macho na wanasiasa wanaokimbilia kwenu, msikubali kutumiwa kwa kulinda maslahi ya wanasiasa, fanyeni kazi zenu za kuwajenga waumini wenu kwa mujibu wa mafundisho ya imani zenu…mkiruhusu kutumiwa na wanasiasa amani ya nchi mutaivuruga”

Alisema ni jambo la faraja kuona viongozi wa dini wanakutana na kuliombea taifa bila kujali tofauti za itikadi zao na kwamba ushirikiano huo unapaswa kuendelea kwa kutoruhusu kugawanywa na wanasiasa.

Mbali ya hilo Membe ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi aliwataka wakazi wa mikoa ya kusini kuhakikisha wanakuwa na haki miliki ya ardhi ili kujilinda na unyang’anyi unaoweza kujitokeza mara mikoa hiyo itakapofunguka kiuchumi.

“Upajikanaji wa gesi mkoani Mtwara ni jambo ambalo litaifanya Mtwara na hata Lindi kuwa sehemu ya mapinduzi ya kiuchumi…ushauri wangu wa bure kwenu ni kuhakikisha munakuwa na haki miliki ya ardhi, vinginevyo mutaporwa ardhi yenu” alishauri waziri huyo

Alifafanua kuwa “Maofisa ardhi  hakikisheni munaongeza kasi ya kupima viwanja na kuwapatia haki miliki wananchi…mikoa hii ya kusini itafunguka kiuchumi na kuwa kimbilio kwa wawekezaji nchini”

Kwa upande wake mbunge Murji, alisema lengo la hafla hiyo ni kuliombea Taifa dhidi ya changamoto mbalimbali zinazolikabili, na kwamba hatua hiyo pia imelenga kuwawezesha viongozi wa dini kukutana na kubadilishana mawazo.

“Nimeona ni heri kwetu kukutana viongozi wote wa dini na kuliombea Taifa ili liepukane na changamoto mbalimbali zinazolikabili…ni muhimu kwa viongozi wa dini kuzingatia ushauri uliotolewa na Waziri Membe ili kunusuru uvunjifu wa amani’ alisema Murji

Mwisho

Advertisements