CUF MTWARA KUANDAMANA KUPINGA GESI KWENDA DAR

CHAMA cha Wananchi (Cuf) mkoani Mtwara kimesema kinaandaa maandamano makubwa kupinga uwamuzi wa Serikali wa kusafirisha gesi

Kisima cha gesi

inayozalishwa mkoani humo kupelekwa Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi.

Uwamuzi huo wa CUF umetangazwa jana na Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho wa Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara, Katani Ahmadi Katani alipokuwa akihutubia mamia ya wakazi wa mji wa Mtwara katika mkutano wa adhara wa uzidunzi wa oparesheni ya ‘amka’uliofanyika  katika Viwanja vya Mashujaa.

Pwani ya Bahari ya Hindi-Sehemu ya Mtwara

Hivi karibuni Serikali ilitangaza nia ya kujenga bomba litakalosafirisha gesi kutoka Visima vilivyopo Msimbati mkoani Mtwara kuelekea Jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, jambo ambalo ilieleza kuwa itasaidia kutatua tatizo la ukosefu wa umeme linalolikabili Taifa kwa sasa.

Katani ambaye alikuwa mgombea ubunge wa tiketi ya chama hicho katika jimbo la Tandahimba na kufanikiwa kuleta ushindani mkubwa katika medali za siasa jimboni humo, alidai uwamuzi huo wa Serikali unalenga kuufanya mkoa wa Mtwara uendelee kuwa masikini abadani.

“Wawekezaji walikuwa wanataka kuja Mtwara kuwekeza kwa sababu kuna umeme wa uhakika unatokana na gesi, leo gesi inapelekwa dare s Salaam sasa hao wawekezaji waje Mtwara kufanya nini? Katika hili hatukubaliani na yupo tayari kwa lolote na hata ikibidi kufa kuhakikisha gesi hii haipelekwi Dar es Salaam” alisema Katani

Alisisitiza kuwa “Hadi sasa hakuna kijiji mbali na vile vilivyokuwa na umeme ambacho kimepata umeme, leo wanatuambia gesi iende dare s Salaam wakati sisi wenyewe tupo kigazi, tunasema hilo haliwezekani …gesi inayopatikana kwenye ardhi yetu ikanufaishe mbali wakati sisi wenyewe mahitaji yetu hayajatosheleza, tuna andaa maandamano makubwa kupinga jambo hili”

Uchimbaji wa gesi

Akiunga mkono jambo hilo Katibu wa CUF wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Saidi Kulaga alisema maandamano hayo yatashirikisha wakazi wote wa mkoa wa Mtwara bila kujali itikadi zao za kisiasa na kwamba watu watakaojitenga nayo, wataadhibiwa kwa kunyimwa ushirikiano na jamii yenzao.

“Sisi tunasema “Mtwara Kwanza”,yule ambaye hatakuwa tayari kushiriki kwenye maandamano hayo, tutamtendanga kwa kila jambo, hata akifiwa na mtoto wake tutamwacha amzike peke yake, kwa sasa yeye hana uchungu na dhuluma wanayofanyiwa wana Mtwara” alisema Kulaga.

CUF na Maandamano

Aidha aliwanyoshea kidole wabunge wa mkoa wa Mtwara kwa kushinda kulipinga suala hilo bungeni na kusisitiza kuwa ni wawakilishi waliokosa wito na uchungu kwa wanaowawakilisha.

Wakati huohuo chama hicho kimeitaka Serikali kuhakikisha ifikapo Februari mwaka huu imewalipa fedha zao wakulima wa korosho ambao wamekopesha korosho zao katika vyama vya msingivya ushirika, chini ya mfumo wa ununuzi wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani.

Katani alisema hadi sasa wapo wakulima wa korosho ambao walipeleka korosho zao ghalani na hawajalipwa asilimia 70 ya bei kama ilivyotangazwa na Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania.

Alisema hali hiyo inasababisha wakulima hao kuishi maisha ya taabu huku wakishindwa kuwatimizia mahitaji muhimu ya shule watoto wao.

“CUF tunasema ifikapo Februari mwaka huu wakulima wote wawe wamelipwa malipo yao ya kwanza na ya pili, vinginevyo tutaongoza wakulima hao kudai haki yao, kupitia maandamano na njia zingine zozote ambazo tutaona ni muafaka kwa wakati huo” alisema Katani

Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania Anna Abdallah kupitia kikao cha Kamati ya Maendeleo na Ushauri ya Mkoa, alikiri kuwapo kwa wakulima ambao hawajalipwa malipo ya awali kama ilivyoamriwa na bodi yake na kwamba tatizo hilo linatokana na kuyumba kwa soko la zao hilo.

Bei ya korosho kwa msimu huu ni sh. 1200 ambapo mkulima alitakiwa kulipwa sh. 850 malipo ya awali ikiwa ni asilimia 70 ya dira ya bei, jambo ambalo halijatekelezwa.

Mwisho