TANECU YANUNUA HISA ZA 200 MIL BENKI NEWALA

CHAMA kikuu cha ushirika cha wilaya ya Tandahimba na Newala, (Tanecu) kimenunua hisa zenye thamani ya sh 200 milioni katika Benki ya Wananchi Newala.

RAis Jakaya Kikwete akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa ghala la TANECU, kushoto ni mwenyekiti wa TANECU Yusuf Nannila

Akiongea na waandishi wa habari mjini Newala jana, mwenyekiti wa Tanecu, Yusufu Nannila, alisema chama cahke kimeamua kununua hisa hizo ili kujiwekea mtaji katika taasisi za kifedha utakaokiwezesha chama hicho kuepukana na mikopo yenye msharti na riba kubwa kutoka taasisi zingine za kifedha.

Alisema ili kuhakikisha wananchi wa wilaya hiyo kupitia vyama vya msingi vya ushirika wa kilimo na masoko wanamiliki benki hiyo, amevitaka vyama vyote 33 vya wilaya hiyo kununua hisa zenye thamani ya shilingi milioni tano kila kimoja.

Mwenyekiti huyo alisema vyama 71 vya wilaya ya Tandahimba ambako tayari benki yao imeanza kutoa huduma vinasubiri maelekezo kutoka kwa uongozi wa benki hiyo ili viweze kununua hisa na kuwa miongoni mwa wamiliki wa benki hiyo

“Iwapo benki hizi zitatengamaa itatuwia rahisi kupata fedha kwaajili ya kuendeshea biashara ya mazao…hivi sasa tunakopa fedha kutoka vyombo vingine ambavyo vinatutoza riba kubwa lakini kama tutamiliki benki hizi tutakuwa na uhuru wa kupanga kiwango cha riba” alisema Nannila.

Nannila alibainisha kuwa chama chake kimefikia uwamuzi huo baada ya kuhamasishwa na kikosi kazi kilichoundwa kwaajili ya kumasisha wananchi wa Newala kununua hisa katika benki hiyo kilichoongozwa na Chitwanga Rashidi Ndembo

Kwa upande wake Ndembo ambaye pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Newala, alisema hisa moja inauzwa kwa sh. 500 na mtu anaruhusiwa kununua kuanzia hisa kumi, ambapo alisema tayari wameshapata kibali kutoka Benki Kuu ya Tanzania kuanzisha mchakato.

“BoT imetuambia ili kuanzisha benki tunatakiwa kuwa na mtaji usiopungua milioni 500 na sisi tumejipanga kuanza na bilioni moja kama mtaji…halmashauri ilikuwa na hisa katika benki ya CRDB tumeuza zote na kununua za benki ya wananchi wa Newala kwa thamani ya shilingi milioni 450 na tutanunua tena kwa milioni 50 ili ifike milioni 500”, alisema Ndembo.

Aidha mwenyekiti huyo alisema kuwa madiwani wote 39 wamekubaliana kununua hisa 200 kila mmoja, vijiji vyote 155 vitanunua hisa 200 na SACCOS saba zitanunua hisa 1000 kila moja ili kufanikisha lengo hilo.

Mwisho.

Advertisements