MADIWANI NUSRA WAZICHAPE KIKAONI

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki walinusurika kuzipiga wenyewe kwa wenyewe kwenye kikao cha baraza la madiwani baada ya kuhitilafiana wakati wa kujadili hoja ya hali ya soko la korosho.

Mwenyekiti wa Tanecu, Yusuf Nannila

Mara baada ya Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Cha Tandahimba, Newala (Tanecu) Daimu Mpakate kuwasilisha taarifa ya hali ya soko la korosho ambayo ilionesha kuyumba, madiwani hao walionekana kujawa na jazba na kuanza kuishtumu Tanecu kwa kushindwa kusimamia vizuri soko la zao hilo.

Mpakate alibainisha kuwa hadi sasa kilo 45,479,465 za korosho zimekusanywa kutoka kwa wakulima ambapo kilo 21,401980 zimeuzwa kwa wanunuzi wakubwa sawa na asilimia 47 na kilo 24,077,485 sawa na asilimia 53 hazijauzwa na zimeendela kuhifadhiwa katika maghala baada ya kukosa wanunuzi.

Katika harakati za kila mmoja kutaka kuchangia hoja hiyo, walijikuta wakihitilafiana wenyewe kwa wenyewe na kuanza kusemeana ovyo, hali iliyoashiria kuwapo kwa uwezekano wa kuzuka vurugu katika kikao hicho.

“Acha kunitisha, we nani…huwezi kunizuia kuhoji … utaniambia nini wewe”ni baadhi ya maeneno yaliyosikika kutoka kwa madiwani hao huku wengi wao wakiwa wameonyosha mikoni juu wakiomba kuchaguliwa kuchagia hoja.

Korosho Nje ya Ghala baada ya kukosa mnunuzi

Mwenyekiti wa kikao hicho Ali Ndingo alilazimika kugonga meza mara kadhaa kutaka utulivu bila mafaniko, hali iliyomlazimu katibu wa kikao hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Abdallah Njovu kusimama na kumaka mwenyekiti wake kutumia kanuni kuwaadhibu wanakiuka utaratibu.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia kanuni unaweza kumtoa nje diwani yeyote ambaye anakwenda kinyume na kanuni tulizojiwekea…haiwezekani watu waongee kana kwamba wahapo kwenye kikao” alisema Njovu

Mwenyekiti wa kikao hicho, Ndingo alitumia dakika kadhaa kuwasihi madiwani hao kuwa na hekima katika kujadili sula hilo huku akikosoa waliochangia kutoa shutma na mapendekezo nje ya mada.

“Jamani inyi sio mkutano mkuu wa Tanecu, masuala munayohoji yanapaswa kuhojiwa na mkutano mkuu wa Tanecu, sisi tuhoji nini hatma ya wakulima wetu kufuatia kuyumba kwa soko la zao hilo, hilo ndilo jukumu letu” alisema Ndingo

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Hasna Mwilima aliwaonya madiwani kuacha tabia ya kuendeleza malumbano yasiyo na tija kwa maendeleo ya wilaya hiyo na kuwataka kuhoji pale mambo yanapokwenda kinyume.

“Niliwaalika Tanecu ili mupate fursa ya kujua hali ya soko la korosho, nilitaraji maswali mengi yalenge kwenye kufahamu nini ufumbuzi wake…tuache malumbano yasiyo na tija, fanyeni kazi mliyotumwa na wananchi” alisema Mwilima

Mwenyekiti wa Tanecu, Yusuf Nannila alisema kuwa jitihada mbalimbali zinafanywa na chama chake kuhakikisha wanapata ufumbuzi wa kuyumba kwa soko la korosho ikiwa pamoja kuuza korosho kwa njia ya mtandao wa kompyuta (Internet)

“Hivi karibuni tutaanza kuuza koroho nje ya nchi kwa kutumia mtandao (internet), ofisa masoko wetu alikuwa masomoni Uganda, na hivi karibuni atarejea kuhakikisha tutaondokana na tatizo hili, ili wakulima wetu wasizidi kuathirika…naomba tuendelee kuwa na subira kwani si tatizo la Mtwara, ni tatizo la korosho Tanzania” alisema Nannila