WANAFUNZI NDANDA WAGOMA KURUDI DARASANI, WADAIWA KUANDAA VURUGU MITIHANI ISIFANYIKE

WANAFUNZI 20 wa shule ya Sekondari ya juu ya Wavulana Ndanda, iliyopo wilayani Masasi mkoani Mtwara, wamegoma kurejea darasani licha ya Serikali kuwafutia adhabu ya kufukuzwa shule kutokana na madai ya kujengwa kwa Msikiti shuleni hapo.

Mufti wa Tanzania Shehe Shaaban Simba

Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia KUSINI  leo na kuthibitishwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Fatma Ally zinasema kuwa wanafunzi hao wamekataa kurejea darasani wakishinikiza serikali iwaombe radhi badala ya kutoa taarifa ya kuwasamehe.

Habari hizo  zinadai kuwa mkuu wa wilaya akiwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya pamoja na viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) mkoa wa Mtwara na wilaya ya Masasi walishindwa kuwashawishi wanafunzi hao kurejea darasani.

“Ni kweli wamegoma kurejea darasani kwa madai serikali iwaombe radhi na sio kuwasamehe…wamesema hawapo tayari kuingia darasani na kufanya mitihani ya kidato cha Sita hadi pale ombi langu la serikali kuwaomba radhi litakapotekelezwa” alisema Ally

Aliongeza kuwa “Waligoma kuongea na sisi licha ya kujitambulisha kwao, walidai hawamtambui mkuu wa wilaya, wamesema kesho hakutafanyika mtihani kwa shule ya Ndanda na wapo tayari kumwaga damu kwa ajili hiyo…hivi ninapoongea tayari waislamu kutoka kona mbalimbali za nchi wamewasili Ndanda kwa ajili ya kuzuia kufanyika kwa mitihani hiyo”

Mkuu huyo wa wilaya alifafanua kuwa tayari waislamu kutoka chuo kikuu cha waislamu cha Morogoro wamewasili Ndanda na wengine kutoka wilaya za mkoa wa Mtwara.

“Wanafunzi wa chuo kikuu cha waislamu cha Morogoro wamefika, wa Masasi, Tandahimba na Mtwara kwa taarifa tulizonazo wamewasili pia….kimsingi hali ni tete sana” alieleza Ally

Jana serikali kupitia Mkuu wa mkoa wa Mtwara Joseph Simbakali ilitoa tamko la kuwataka wanafunzi waliofukuzwa shuleni hapo kurejea mara moja ili waweze kufanya mitihani ya kidato cha sita na kuwataka wafuate sheria na kanuni za shule katika kipindi chote cha mitihani yao.

Wanafunzi hao walifukuzwa shule 21 Desemba mwaka jana na kwamba kamati ya rufaa iliketi Januari 31 mwaka huu na kuridhia wanafunzi hao warejee shule.

mwisho

Advertisements