HALI YA USALAMA TETE NDANDA,13 WAGOMA KUFANYA MITIHANI

HALI ya usalama katika kijiji cha Ndanda wilaya ya Masasi, mkoani
Mtwara imeendelea kuwa tete kufuatia idadi kubwa ya waislamu kuendelea
kuwasili katika moja ya Msikiti uliopo kijijni hapo huku wanafunzi 13
wa kidato cha sita shule ya sekondari Ndanda ambao ni waislam
wakiripotiwa kugoma kufanya mitihani.

Juzi ilidaiwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya hiyo, Fatma Ally kuwa
waislam kutoka sehemu mbalimbali za nchi na mkoa walikuwa
wanakusanyika katika moja ya msikiti uliopo Ndanda wakijiandaa kufanya
vurugu kwa lengo la kuzuia kufanyika kwa mitihani hiyo.

Hata hivyo kinyume na ilivyotarajiwa, mitihani hiyo imeendela
kufanyika shuleni hapo katika hali ya utulivu na amani.

KUSINI ilifika Ndanda na kukuta hali ni shwari huku polisi
waliojiandaa kukabiliana na vurugu wakiwa katika magari wakidhurura
mitaani hali iliyoongeza hofu kwa wakazi wa kijiji hicho.

Pia KUSINI ilishuhudia makundi ya Waumini wa Kiislamu wakielekea
msikitini hapo kwa miguu na wengine kwa magari hali ambayo haijaweza
kufahamika mara moja nini kusudio la mkusanyiko huo.

Juhudi za kumpata msemaji wa waislamu hao hazikuzaa matunda baada ya
kukataa kuhojiwa, na kuamru waandishi wa habari kuondoka mara moja
katika eneo hilo la Msikiti.

Mkuu wa shule ya Ndanda Joseph Sowani amethibitisha wanafunzi hao 13
kutofanya mitihani yao licha ya serikali kuwaruhusu.

“Wanafunzi wa kidato cha Sita waliofukuzwa shule walikuwa 14, mmoja
alirejea shuleni baada ya rufa yake kukubaliwa…hawa 13 hawakukata
rufaa na hata serikali ilipowaruhusu kurejea shuleni ili waweze
kufanya mitihani yao hakuna aliyefika” alisema Sowani

Aliongeza kuwa “Hali ya usalama ni swari hadi sasa, wanafunzi
wanaendelea vizuri na mitihani….wanafunzi 470 wanafanya mitihani kwa
sasa”

Shehe wa Kata ya Mwena Seif Ali ambaye pia ni imamu wa msikiti huo
alisema hajui dhumuni la wasilamu hao kuendelea kukusanyika msikitini
hapo na kwamba alitoa taarifa polisi ili kuimarisha usalama.

“Wanafunzi na waislam wengine wapo pale msikiti, sijui wanasubiri
nini…nilitoa taarifa polsi hata hivyo bado wapo Msikitini hapo,
sijui wanataka kufanya nini.

Mmoja wa waumini wa Kiislamu kwa sharti la kutotajwa jina alisema
wanafunzi hao hawawezi kufanya mitihani kwa sababu wamekaa nyumbani
kwa muda mrefu bila kujisomea kutokana na uwamuzi wa bodi ya shule wa
kuwafukuza.

“Wanafunzi wana zaidi ya miezi miwili hawajaingia darasani, leo
unamwambia aende kufanya mitihani, hivi hii si mbinu ya kuwafelisha
ili waislamu waendee kukosa elimu bora” kilihoji chanzo chetu

Waislam hao wameingia katika mgogo baada ya wanafunzi 19 kufukuzwa
shule 21 Desemba mwaka jana kutokana na madai ya kujengewa msikiti
shuleni hapo, sanjari na kutuhumu uongozi wa serikali ya wanafunzi
uliwekwa madarakani kwa misingi ya kidini.

Baadhi ya wananchi wameelezea hofu yao kufuatia kuendela kuwasili kwa
makundi ya waislamu kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa.

“Sijui wanataka kufanya nini, maana ukienda pale Msikitini muda wote
utawakuta wanaswali…kinachotutia hofu ni kule kuendelea kuwasili kwa
waislamu wengine , tunajiuliza wakiwa wengi wanataka kufanya nini”
alisema Kelvin Mkazi wa Ndanda
Mwisho

Advertisements