MWANDISHI ITV APIGWA NDANDA

MWANDISHI wa bahari wa ITV na Redio One mkoani Mtwara, Modestus Mwambe amepigwa na kundi la Waislamu waliopiga kambi Ndanda wilayani Masasi, mkoani Mtwara wakipinga hatua ya serikali ya kuwarejesha shuleni wanafunzi wa kidato cha Sita siku mbili kabla ya kuanza kwa mitihani ya kitaifa.

Habari zilizoifikia KUSINI zinaeleza kuwa tukio hilo la kusikitisha limetokea leo, saa 11 asubuhi baada ya Mwandishi huyo mkongwe kwenda Msikitini walikopiga kambi waislamu hao kuwahoji juu ya sakata nzima.

Habari zinasema kuwa Mwandishi huyo hakuwahi kuwahoji wahusika kwani wakiwa katika mahojiano ya kujitambulisha, alilakiwa na ‘vibao’ kutoka kwa waumini hao kisha kumpora kamera na kumwachia huku akiugulia maumivu.

“Ni kweli nimepigwa na kunyang’anywa kamera, ila sijaumia sana na ninaendelea vizuri, nimetoa taarifa polisi na sasa wanashughulikia suala hilo” alisema Mwambe akiongea kwa simu na KUSINI

Mkuu wa shule ya Ndanda Joseph Sowani alithibitisha kuhojiana na mwandishi huyo saa 10 asubuhi ya leo na kwamba alimuonya asiende kuhojiana na waislamu hao kwani anaweza kuhatarisha usalama wake.

“Baada ya kumaliza mahojiano hapa alisema anakwenda msikitini, mimi nikamuonya kuwa asiende kwani anaweza kuhatarisha usalama wake…baadae napata taarifa kuwa mwandishi huyo amepiga na kunyang’anywa vifaa vyake vya kazi” alisema Sowani

Jumla ya wanafunzi 13 wa kidato cha sita shule ya sekondari Ndanda wamegoma kufanya mitihani ya kumaliza masomo yao kwa madai serikali ilichelea kutoa tamko la kuwarejesha na kwamba hawakujiandaa kwa ajili mitihani hiyo.

Wanafunzi hao ni miongoni mwa 19 waliofukuzwa shule desemba, 21 mwaka jana kufuatia madi ya kutaka kujengewa Msikiti shuleni hapo na kushtumu uongozi wa serikali ya wanafunzi umewekwa madarakani kwa misingi ya kidini.

Mwisho

Advertisements