BARABARA MTWARA, TANDAHIMBA, NEWALA HADI MASASI KUTOJENGWA KWA LAMI

BARABARA ya kutoka mjini Mtwara hadi wilayani Masasi kupitia Tandahimba na Newala haitajengwa kwa kiwango cha lami katika kipindi cha 2010/15 na badala yake itafanyiwa upembuzi yakinifu pekee.Imebainika.

Sehemu ya barabara ya Mtwara tandahimba ikifanyiwa matengenezo

Kwa nyakati tofauti wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, viongozi mbalimbali wa CCM akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais Dk. Mohamedi Bilal waliwahakikishia wananchi wa mkoa wa Mtwara kuwa ndani ya kipindi hiki cha miaka mitano barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 209 itajengwa kwa kiwango cha lami na kwamba imo katika Ilani ya chama.
 
Katika kikao cha Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Mtwara kilichoketi hivi karibuni wilayani tandahimba, mkoani hapa kupitia utekelezaji wa Ilani ya chama hicho, katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2011 chini ya mwenyekiti wake, Alhaji Dadi Mbullu wajumbe walipokea taarifa kuwa katika kipindi cha miaka mitano (2010/15) barabara hiyo haitajengwa kwa kiwango cha lami na badala yake itafanyiwa upembuzi yakinifu pekee.
 
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa taarifa hiyo ilitolewa na Mbunge wa Mtwara Mjini, Asnein Murji akidai kwamba kinyume na Ilani ya uchaguzi inayotamka ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami katika kipindi hiki cha miaka mitano, serikali imebadili msimamo huo.
 
“Kwa taarifa mwenyekiti ni kwamba, barabara yetu kwa miaka mitano ni upembuzi yakinifu tu, hakuna lami itakayowekwa kwa kipindi hicho…sasa mimi nitoe ombi maalum la kuundwa kamati ya kwenda kuonana na rais (Jakaya Kikwete)…si wabunge wala mawaziri watakaoweza kumshawishi na kumueleza umuhimu wa barabara hii” alisema Murji
 

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Jakaya Mrisho katika moja ya mikutao yake ya kampeni mkoa Mtwara mwaka 2010

Aliongeza kuwa “Barabara hii ndiyo muhimili wa uchumi wa mkoa wa Mtwara, korosho zote zinasafirishwa kupitia barabara hii na unapozungumzia siasa Mtwara ni lazima uguse barabara hii, isitoshe imo katika Ilani ya utekelezaji wa chama kwa kipindi hiki, leo tutawaambia nini wananchi waliojawa na matumaini ya mda mrefu kuona barabara ya yao ikijengwa kwa lami?”
 
Kwa mujibu wa chanzo chetu ambacho hakikutaka kutajwa gazetini, hoja hiyo iliwashtua wajumbe wengi ndani ya kikao hicho na kupendekeza kuundwa kwa kamati teule ya kuonana  na Rais Kikwete ili kubadaili msimamo huo wa serikali.
 
“Tumeshtushwa sana na taarifa hizi, leo hii hatuna la kuwaambia wananchi wetu… tumeiomba sekretarieti ya mkoa kuangalia uwezekano wa kuunda kamati teule ili kuonana na rais juu ya jambo hili, ni jambo nzito sana , linaloweza kutuathiri kisiasa mkoani kwetu’ kilisema chanzo chetu.
 
Katibu wa CCM wa mkoa wa Mtwara, Alhaji Masoud Mbengule alithibitisha wajumbe wa kikao hicho kupokea taarifa hiyo kutoka kwa Mbunge Murji na kueleza kuwa ofisi yake haijapata barua rasmi ya mabadiliko hayo ya utekelezaji wa Ilani, hivyo haiwezi kuunda kamati hiyo teule.
 
“Ni kweli suala hilo lilijadiliwa kwenye kikao hicho, lakini mimi sijapokea taarifa kwa maandishi juu ya mabadiliko ya Ilani, ninachosema mimi hilo nilisikia kwenye kikao ila sina taarifa naomba mninukuu hivyo, siwezi kuunda kamati kwa maneno ya kusikia, nitaulizwa nimetoa wapi hiyo kauli” alisema Alhaji Mbengule
 
Alisisitiza kuwa “Hadi sasa ninachokifahamu ni kwamba Ilani ya uchaguzi itatekelezwa kama ilivyo na hakuna mabadiliko, ila tumeomba serikali itekeleze haraka ahadi hii ya ujenzi wa barabara ya lami maana inahitajika sana , kutokana na umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi”
 
Sanjari na hilo halmashauri hiyo imekataa kupokea ukarabati wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe kwa madai Mkandarasi anaongeza ubovu badala ya kutatua tatizo
 
“Ajabu ilioje, mahala ilipokarabatiwa ndipo pabovu zaidi, Mkandarasi anabeba tope na kuweka barabarani badala ya kuweka kifusi cha changarawe, hii barabara kwa sasa haipitiki kwa urahisi” alisema Suleimani Mtalika Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
 
Katika kikoa hicho cha kawaida cha halmashauri kuu ya CCM mkoa kilikuwa kinajadili utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2011, ambapo pia kilitoa tamko la kukataa ukarabati wa barabara hiyo na kumuagiza Mkuu wa Mkoa kuzungumza na Wakala wa Barabara mkoani hapa (Tanroads) ili kutatua tatizo hilo.
Mwisho
 
Advertisements