WANANCHI WAPAMBANA NA POLISI MTWARA

BAADHI ya wananchi wa mtaa wa Magomeni, Manispaa ya Mtwara-Mikindani juzi jioni walifunga barabara kwa kuweka magogo, kuchoma moto matairi ya magari katikati ya barabara na kurusha mawe magari yaliyojaribu kupita maeneo hayo.

Polisi na magari yao wakijiandaa kukabili vurugu

Barabara zilizofungwa kwa muda ni ya Mtwara mjini kwenda Lindi na yingine ya Mtwara mjini kwenda Tandahimba, wakishinikiza kuachiwa kwa waganga wawili wa jadi wanaojishughulisha na utoaji uchawi baada ya kukamatwa na polisi.

Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za mpira ili kutawanya wananchi hao, vurungu ambazo zilidumu kwa takribani saa moja na nusu.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, vurugu hizo zilianza saa 11 jioni ambapo kundi kubwa na watu lilizagaa barabarani na kuanza kufunga barabara kwa kutandika madodo, kuchoma tairi za magari moto na kuanza kurusha mawe magari yaliyokuwa yanapita maeneo hayo, hali iliyosababisha eneo hilo kutawaliwa na vurugu.

“Kulikuwa na waganga wanaotoa uchawi katika eneo la Mangamba, walipofika karibu na nyumba ya kigogo mmoja, mara polisi walifika na kuwakamata waganga…sisi tunahisi polisi wanatumiwa kulinda maslahi ya wachache” kilisema chanzo chetu cha habari ambacho hakikutaka kutajwa jina.

Aliongeza kuwa “Wananchi walikasirishwa na kitendo hicho na ndipo walipomaliza asira zao kwa kufanya haya unayoyaona ….walikwenda mpaka Mkanaledi ambako kulikuwa na mhadhara wa dini ya kiislam unaondeshwa na Sheikh Mazinge na kufanya vurugu” kilidokeza.

Akizungumza kwa niaba ya kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, mmoja wa maofisa wa polisi mkoani hapo, Focas Malengo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa watu 15 wakiwemo waganga wa jadi wawili wametiwa mbaroni.

Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Ali Hamisi (18) na Fatuma Malimba (57) wote waganga wa jadi ambao walikamatwa eneo la Magomeni mjini hapa baada ya kupokea taarifa kutoka kwa raia mwema juu ya kutaka kuendesha shughuli zao bila ridhaa yake.

Wengine ni Ramadhan bakari (14) mwanafunzi wa shule ya msingi Magomeni, Bakari Makunguli, Mustafa Bakari, Mwihidini Yasini (20), Salm Monokota (20) wote wanafunzi wa sekondari, wakati Saimoni Amidu (34) Amon Mtengera (23), Seleman Stamili (33) Ahamadi Rushuti (16), Juma Mohamedi (16), Hija Makaranga (22), Fadhili Mohamedi (33) na Francis Evaristus (22) wakazi wa Magomeni.

“Tumewakamata watu 15 kuhusiana na tukio hilo…naomba niseme kuwa sisi polisi hatutumiwi na mtu yeyote kulinda maslahi yake, tunachosema vitendo vya utoaji wa uchawi ni kinyume cha sheria” alisema Malengo

“Katika zile vurugu hakuna aliyeripotiwa kujeruhiwa, kama yupo basi ajitokeze…yapo magari ambayo ayamevunjwa vioo likiwemo la Sheikh Mazinge…askari walifanya kazi usiku huohuo na kurejesha hali ya amani” alisisitiza ofisa huyo

Hiyo ni mara ya pili kwa wananchi kupambana na polisi mkoani mtwara kufuatia jeshi hilo kukataza vitendo vya utoaji uchawi vinavyoendeshwa na waganga wa daji na kubarikiwa na wananchi wenyewe ambao huchangia wastani wa sh. 2000 hadi tatu kugharamia shughuli hizo.

Katika tukio la kwanza wananchi walichoma moto pikipiki ya polisi na kujeruhi askari kadhaa.

mwisho

 

Advertisements