RC LINDI AKATAA KUOMBA CHAKULA CHA NJAA

MKUU wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila amesema hayupo tayari kuomba msaada wa chakula kutoka Serikalini kwa ajili ya watu wanaokabiliwa na njaa mkoani humo.https://kusini.files.wordpress.com/2012/02/02.jpg?w=300

Mkuu wa mkoa wa Lindi Ludovick Mwananzila (wa pili kushoto) akiwa na viongozi mbalimbali wa serikali mkoani Lindi, wa kwanza kushoto aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Saidi Sadick

Mwananzila ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akifungua kikao cha kamti ya ushari ya mkoa huo (RCC), ambapo alisisitiza kuwa hakuna sababu ya msingi ya mkoa huo kushindwa kujitosheleza kwa chakula.

Kauli hiyo imekuja wakati taarifa ya Mshauri wa Kilimo wa mkoa huo, John Likango ikieleza kuwa jumla ya kaya 8000 mkoani humo zinakabiliwa na upungufu wa chakula kwa msimu huu wa kilimo.

“Waheshimiwa Wabunge naomba munielewe sitaomba chakula cha njaa…sifanyi kazi hiyo…maelekezo tumepeana namna ya kusimamia kilimo, ni lazima tuhakikishe wakulima wanazalisha chakula cha kutosha kujilisha kwa miezi 12 na ziada” alisema Mwananzila

Alisisitiza kuwa “Kama wilaya moja ina njaa basi waombe msaada kutoka kwenye wilaya nyingine jirani iliyojitosheleza kwa chakula sio mimi kwenda kuomba chakula serikalini, sifanyi kazi hiyo”

Alifafanua kuwa yupo tayari kufanya hivyo iwapo kutajitokeza ukame kwa eneo kubwa la mkoa huo na majanga mengine ambayo yanaweza kuathiri kwa kiwango kikubwa shughuli za kilimo.

“Hatuna sababu ya kutojitosheleza kwa chakula, ardhi ipo, mvua zinanyesha, kwa nini sasa tuwe ombaomba kila mwaka…nawaomba sana kukuzingatia maelekezo tuliyopeana katika kusimamia kilimo kwa wananchi wetu” alisema mkuu huyo wa mkoa.

Akiwasilisha taarifa ya kilimo katika kikao hicho, Likango aliwaeleza wajumbe kuwa shughuli za kilimo kwa msimu 2011/12 zinaendelea vizuri na kwamba hadi sasa ni kaya 8000 zilizoripotiwa kuwa na upungufu wa chakula.

“Kaya 8000 zina upungufu wa chakula hadi sasa, kaya hizi zimetawanyika katika maeneno mbalibali ya mkoa, kutokana na uzalishaji wa kuridhisha wa mazao ya chakula kwa msimu uliopita tatizo hili linaweza kutatuliwa ndani ya mkoa wetu” alisema Likango

Mwisho

 

Advertisements