MWANDISHI ALIYEPIGWA ALITAKA KUINGIA NA VIATU MSIKITINI

Jengo la Msikiti

MWANDISHI wa habari wa ITV na Redio One mkoani Mtwara, Modestus Mwambe alipatwa na makasa wa kuchapwa makofi na kundi la Waislamu katika moja ya Msikiti uliopo Ndanda wilayani Masasi mkoani hapa baada ya kutaka kuingia Msikitini humo huku akiwa amevaa viatu. Imebainika

Mwambe alikwenda Msikitini hapo kuhojiana na kundi hilo la Waislamu wanaopinga kufukuzwa shule kwa wanafunzi Waislamu 19 wa shule ya sekondari ya wavulana Ndanda (Ndanda boys high school)) na baadae kutenguliwa kwa adhabu hiyo siku chache kabla ya kuanza kwa mitihani ya kuhitimu kidato cha Sita.

Kwa mujibu wa imani ya Kiislam mtu hawezi kuingia Msikitini akiwa amevaa viatu, hivyo viatu huvuliwa kabla ya kuingia Msikitini, kinyume inavyodaiwa kufanywa mwandishi wa habari huyo.

Uchunguzi uliofanywa na KUSINI hivi karibuni umebaini kuwa waumini hao walichukizwa na kitendo cha mwandishi huyo kutaka kwenda kinyume imani yao na ndipo walipomteremsha kwenye ngazi za kuingia msikitini huo kwa makofi.

“Ni kweli nimepigwa na kunyang’anywa vifaa vyangu vya kazi (Kamera)….nimeripoti polisi na wanalishughulikia” alithibitisha Mwambe kutokea kwa tukio hilo alipohojiwa na KUSINI.

Baadhi ya vyanzo vya habari kutoka Msikitini humo vimeeleza kuwa Mwandishi huyo nguli wa habari mkoani hapa alitaka kuongea na kiongozi wa wasilamu hao, ambao waliweka masikani yao ndani ya msikiti huo.

“Kosa alilofanya yule mwandishi ni kutaka kuingia masikitini akiwa amevaa viatu….waislamu walichukizwa na kitendo hicho na ndipo walipomwadhibu kwa kumchapa makofi” kilisema chanzo chetu.

KUSINI inalaani vitendo vya upigaji na unyanyasaji wa Waandishi wa Habari kwani vinaweza kufifisha uhuru wa upatikanaji na utoaji wa habari.

 

Advertisements