TANI 16626 ZA KOROSHO ZADODA LINDI

ZAIDI ya tani 16626 za korosho zipo katika maghala mbalimbali yanayotumika  kuhifadhi zao hilo mkoani Lindi baada ya kukosa wanunuzi.

Kiasi hicho cha korosho ni kati ya tani 32580 zilizokusanywa kutoka kwa wakulima mkoani humo, ambapo kiasi cha tani 15954 zimeuzwa kwa wanunuzi wakubwa huku kiasi kilichobakia kikiendelea kusota maghalani pasi ya wanunuzi.

Hali hiyo inadaiwa kusababishwa na wanunuzi wa zao hilo kufanya mgomo baridi wa kutonunua kwa lengo la kudhoofisha soko ili wanunue chini ya bei dira ya sh.1200 ambapo mkulima hulipwa asilimia 70 malipo ya awali.

Tayari Serikali kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ilitoa siku 14 hadi kufikia Februari 18 wanunuzi wote wa zao la korosho wawe wamenunua vinginevyo wangefutiwa vibali vyao vya ununuzi wa zao hilo.

Akiwasilisha hali ya soko la korosho katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Lindi (Rcc) kilichofanyika mjini Lindi mwishoni mwa wiki, mshauri wa kilimo sekretarieti ya mkoa huo, John Likango alisema kufuatia hali hiyo wapo wakulima ambao hawajalipwa sh. 850 kwa kilo kama malipo ya awali ya dira ya bei ya sh. 1200

“Mheshimiwa mwenyekiti hadi sasa ni tani 15954 ndizo zilizonunuliwa wakati tani 16626 zipo katika maghala baada ya kukosa wanunuzi…hali ya soko la korosho ni mbaya sana…wakulima wapo ambao hawajalipwa malipo ya kwanza hadi sasa, ni wajibu wetu kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao” alisema Likango

Akifafanua hoja hiyo Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila alisema hali ya soko la korosho ni tete na kwamba mkoa unasubiri uwamuzi wa serikali baada ya siku 14 walizotoa kwa wanunuzi wa zao hilo kwisha bila ya mafanikio.

“Makampuni 57 yalijiandikisha kununua korosho kwa msimu huu, 19 yalikwenda sokoni na kati ya hayo tano tu ndiyo yanayosafisha nje ya nchi…ukichunguza utabaini kuwa makampuni mengi ya watu wa kati na ndio hao wanaoyumbisha soko” alisema Mwananzila

Akionesha kukerwa na tatizo hilo mkuu huyo wa mkoa alisema “Wengine wanaotukwaza ni viongozi wenzetu waliojiingiza kwenye biashara hii…hawana huruma na wananchi…tunajua wanachokifanya”

Mbunge wa Kilwa Kusini Seleman Bungala (CUF) maarufu Bwege licha ya kusifia mfumo wa stakabadhi ghalani alisema hautakuwa na tija iwapo utashindwa kuhakikisha wakulima wanapata haki yao.

“Sisemi mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ni mbaya, ila iwapo wakulima wataendelea kukosa haki yao, mfumo huu utakuwa hauna tija kwa wakulima…naomba kujua lini wananchi wangu watapata fedha zao za malipo ya awali?” alihoji Mbwege

Mwisho