UMWAGILIAJI KANDA KIKWAZO LINDI

Moja ya shmba la Umwagiliaji mkoani Lindi

OFISI za Umwagiliaji kanda ya kusini, zilizopo mkoani Mtwara zimedaiwa kuwa ni kikwazo cha utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji mkoani Lindi.

Tuhuma hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki na wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa wa Lindi katika kikao chao (RCC) kilichoketi mjini Lindi chini ya mkuu wa mkoa huo, Ludovick Mwananzila.

Wajumbe hao walitoa shutma hizo mara baada ya ofisa kilimo wa mkoa huo, John Likango kuwasilisha taarifa ya kilimo, iliyoonesha kuwa utekelezaji wa miradi mingi ya umwagiliaji umekuwa hafifu kutokana na kukosekana kwa wataalam wa kusimamia kwa karibu wakati wa ujenzi wa miradi hiyo.

“Moja ya changamoto katika miradi ya umwagiliaji ni kukosekana kwa wataalam wanaosimamia kwa karibu wakati wa ujenzi wa mabwawa…tunategemea wataalam kutoka ofisi za kanda zilizopo Mtwara” alisema Likango

Mbunge wa Liwale, Faith Mitambo aliunga mkono taarifa kwa kutolea mfano wa mradi wa umwagiliaji wa Ngongowele wilayani Liwale ambao aliusimamisha ujenzi baada ya kutoridhishwa na maendeleo yake.

“Zaidi ya milioni 800 zimetumika, ukiangalia mradi wenyewe hauleti matumaini…mimi naona bora serikali ituletee watalaam, ambao watawajibika kwetu” alisema Mitambo

“Nilipofika pale sikuridhishwa na utekelezaji wa mradi nikaamua kuusimamisha…mkuu wa mkoa nakuomba ufike kwenye ule mradi ujionee mwenyewe…hatuwezi kufika kwa mwendo huu” alisisitiza mbuge huyo

Mkuu wa mkoa wa Lindi, Mwananzila aliungana na wajumbe kwa kueleza kuwa ni vigumu kwa mkoa huo kupiga hatua katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji iwapo utaendelea kutegemea wataalam kutoka ofisi za kanda zilizopo mkoani Mtwara.

“Eneo lao la utawala ni kubwa kiasi hawawezi kulisimamia kikamilifu, tuiombe serikali ifungue na ituletee wataalam wa umwagiliaji hapa Lindi, haya mambo ya kanda yanatuyumbisha” alisema Mwananzila

Wajumbe wa kikao hicho kwa pamoja waliafikiana kuiomba serikali kufungua ofisi ya umwagiliaji katika mkoa huo ili kusogeza huduma kwa wananchi na kurahisisha utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji.

Mwisho

Advertisements