SANGOMA ADAIWA KUMTOROSHA, KUMBAKA MWANAFUNZI MGONJWA

POLISI mkoani Mtwara inamshikilia mganga wa jadi (Sangoma), Mussa Juma (20) mkazi wa kijiji cha Nyangamala mkoani Lindi kwa tuhuma za kumtorosha na kumbaka mgonjwa ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha nne aliyekwenda kupata matibabu nyumbani kwake.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Maria Nzuki aliwaambia waandishi wa habari mkoani hapa jana kuwa mgonjwa huyo (17) ni mwanafunzi wa kidato cha nne, moja ya shule za sekondari mkoani hapa, ambapo jina lake na shule vimehifadhiwa.

Akihadhithia mkasa huo Kamanda Nzuki alisema Desemba mwaka jana mganga huyo alikwenda Msangamkuu Manispaa ya Mtwara-Mikindani nyumbani kwa Athumani Ibrahimu (65) baada ya kuitwa na mkewe Ibrahimu, aliyemtaja kwa jina la Fatuma Mohamedi (35) kumtibu mtoto wao anayesumbuliwa na maradhi ya kuanguka na kupoteza fahamu.

“Ibrahimu alipomwangalia mganga akaanza kumtilia shaka hivyo alimtimua…mganga aliwaambia binti na mama yake kuwa ana eneo analotumia kutibia huko Mikindani, hivo binti huyo apelekwe huko na ndipo mama kwa siri alimpeleka Mikindani binti yake ili atibiwe bila ya baba yake kujua” alisema Kamanda Nzuki

Alifafanua kuwa “Huko Mikindani mganga alimpa dawa na kumtaka kimapenzi na baadaye kumbaka … mganga aliamua kumtorosha  mwanafunzi huyo hadi Mingoyo-Mnazimoja mkoani Lindi na kuishi naye kama mume na mke…

Wazazi wake walipowasiliana na mtoto wao alikuwa anawaambia mganga amemwambia kuwa wao ndiyo walikuwa wanamroga hivyo hawezi kurudi”

Alibainisha kuwa Ibrahimu alikwenda kutoa taarifa polisi Februari 19, mwaka huu katika kituo cha polisi Mikindani kuomba msaada na ndipo polisi walipomsaka na kufanikiwa kumkamata huko Mingoyo akiwa na mtoto huyo na mabinti wengine 14 waliokuwa wakiendelea kutibiwa na mganga huyo.

“Mganga huyo alikamatwa nyumbani kwa Mwanaidi Omary (23) akiendelea na shughuli zake za kutoa tiba, mwenyeji wake huyo alithibitishia polisi kuwa mganga huyo alikuwa akiishi na binti aliyemtorosha kama mke na mume” alifafanua Nzuki

Aliongeza kuwa “Binti mwenyewe amekiri kubakwa mara kadhaa na mganga huyo bila ya kutumia kondom … kila alipojiandaa kurudi kwao alikuwa akipumbazwa na kujikuta akighairi…mganga mwenyewe amekiri kuendesha shughuli za uganga bila kibali”

Alieleza kuwa baada ya kukamatwa binti huyo alikutwa na mafuta na vipodozi vinavyodaiwa kununuliwa na mganga huyo, huku mganga kikamatwa na tunguri alizokuwa anatumia kutoa tiba.

Alisema kukamatwa kwa mganga huyo kumetokana na ushirikiano baina ya polisi wa Mtwara na wa Lindi na kwamba kwa sasa mtuhumiwa amerejeshwa Mtwara kujibu madai yake ya msingi kabla ya kupelekwa mkoani lindi ambapo amefunguliwa shtaka la kufanya tiba ya kienyeji bila kibali.

Kamanda Nzuki ametoa wito kwa wananchi mkoani Mtwara kushirikiana na jeshi lake kuwabaini waganga matapeli ambao wamekuwa wakichonganisha na kupandikiza chuki miongoni mwa jamii ili wachukuliwe hatua.

mwisho