ULEDI WA CUF MTWARA AJITOA UANACHAMA

ALIYEKUWA mgombea ubunge jimbo la Mtwara mjini kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) kwenye uchaguzi wa mwaka 2010, Uledi Hassan Abdallah amejivua uanachama wa chama hicho.

Uledi (34) amekabidhi barua ya kujivua uanachama kwa Mwenyekiti wa CUF tawi la Mzambarauni, kata ya Likombe, wilaya ya Mtwara mjini Saidi Mtanga Februari, 25, mwaka huu.

Akielezea sababu za kujivua uanachama, amesema kuwa haridhishwi na mwenendo wa CUF kitaifa na kiwilaya. Ameongeza kuwa chama kinamomonyoka kutokana na kufukuzwa kwa mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed.

Alisema kuwa wakati wa kampeni za kugombea ubunge mwaka 2010, pamoja na kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo ambapo mbunge wa Mtwara mjini Asnein Murji  (CCM) alishinda, yeye hakupata msaada wa kutosha kutoka kwa chama.

“Siridhishwi na mwenendo wa chama kitaifa na kiwilaya… gharama zote za kampeni na kesi zilitolewa na wana-Mtwara, CUF Taifa haikuwa na msaada wowote” alisema Abdallah.

Alisema kuwa kwa sasa hajaamua hatima yake ya kisiasa, ila anaangalia na kusikiliza mahitaji na maoni ya wananchi na ndipo atakapotoa uamuzi kuona hatua gani achukue, kama kujiunga na chama kingine au kuachana na siasa.

Alisema kuwa ameongea na baadhi ya viongozi waliojiengua CUF ambao inadaiwa wana mpango wa kuanzisha chama cha siasa, ila hajaamua bado kama anaweza kujiunga nao.

Uledi Abdallah alijiunga na CUF mwaka 2000 katika tawi la Chemchem, Kinondoni, mkoani Dar es Salaam. Alihamia tawi la Mzambarauni, kata ya Likombe, wilaya ya Mtwara mjini mwaka 2010 na kupata nafasi ya kugombea ubunge jimbo la Mtwara mjini kupitia tiketi ya chama hicho.

Kuhusu muelekeo wa siasa, ametoa ushauri kuwa wana-Mtwara na watanzania kwa ujumla waache mazoea ya kuchagua viongozi kwa kuangalia vyama, bali waangalie sifa za wagombea bila kujali vyama vyao. Wapime uwezo wa mgombea wa kuwatumikia wananchi anaotaka kuwawakilisha, kwani mtu ndiye anayewakilisha, si chama.

Mwisho

 

Advertisements