CUF MTWARA YAPARAGANYIKA

BUNDI ameendelea kuwika ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) baada ya viongozi wote wa chama hicho Manispaa ya Mtwara-Mikindani kujiuzulu.

Kabla ya kutangaza kujiuzulu kwa uongozi huo jana, Mwenyekiti wa CUF Manispaa ya Mtwara-Mikindani Salum Mchimbuli alitangaza kuvunja kurugenzi zote za chama hicho na kuhitimisha kazi hiyo kwa kujiuzulu yeye mwenyewe.

Hatua hiyo imekuja siku mbili tangu aliyekuwa mgombea wa ubunge wa chama hicho Mtwara mjini, Uledi Abdallah kutangaza kujivua uanachama kwa kile alichokidai kuwa chama hicho kina mwelekeo wa kufa kwa sasa hivyo hawezi kufa nacho.

KUSINI ilidokezwa kuwa uongozi huo ulifikia hatua hiyo baada ya kulazimishwa na kundi la wanachama waliovamia ofisi za chama hicho zilizopo eneo la mashujaa mjini hapa na kuwakuta viongozi hao wakiendelea na kikao cha ndani ambacho kilikuwa kinajadili pamoja na mambo mengine uwamzi wa Uledi kujiondoa uanachama.

“Wakati viongozi wanandelea na kikao cha ndani, ghafla kundi la watu waliojitambulisha kuwa ni wanachama CUF walivamia ofisi na kutaka kufanya vurugu, mwenyekiti aliwauliza wanataka nini na ndipo walipomshinikiza avunje kurugenzi zake zote na mwenyewe ajiuzulu” kilisema chanzo chetu kilichoudhuria kikao hicho kwa sharti la kutotajwa jina

Mwenyekiti wa chama hicho Mchimbuli, alipotafutwa na KUSINI ili aweze kutolea ufafanuzi suala hilo , hakupatikana kwenye simu yake ya mkononi.

Hata hivyo aliyekuwa katibu wa chama hicho, Saidi Kulaga amethibitisha kuvunjwa kwa kurugenzi zote zilizokuwa chini yake na kujiuzulu kwa mwenyekiti wake huku akisema kuwa “Mwenyekiti alitumia busara ili kuepusha madhara”

“Walifika vijana zaidi ya 30 hivi, walikuwa wamehamaki, tayari kufanya lolote, hivyo mwenyekiti aliwauliza nini wanataka na kisha kutekeleza matakwa yao …kilichotokea ni kinyume na Katiba ya chama, Katiba imeweka utaratibu wa namna ya kuwaondoa viongozi madarakani, si kama uliofanywa na vijana hao” alisema Kulaga

Alibainisha kuwa vijana hao waliushhtumu uongozi wa CUF wilaya kuwa, umesababisha aliyekuwa mgombea ubunge kwa chama hicho, (Uledi) kujivua uanachama.

“Sisi hatujajiondoa kwenye chama, ni wanachama halali wa CUF ila sio viongozi tena…baadae tutangalia Katiba inasemaje katika mazingira hayo…mengine ni mambo ya ndani siwezi kusema” alisisitiza Kulaga

Uledi (34) alikabidhi barua ya kujivua uanachama kwa Mwenyekiti wa CUF tawi la Mzambarauni, kata ya Likombe, Manispaa ya Mtwara-Mikindani, Saidi Mtanga Februari, 25, mwaka huu.

Akielezea sababu za kujivua uanachama, alisema kuwa alitelekezwa wakati wa kampeni za kugombea ubunge mwaka 2010, pamoja na kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo yaliyompatia ushindi mnono Asnein Murji (CCM).

“Siridhishwi na mwenendo wa chama kitaifa na kiwilaya… gharama zote za kampeni na kesi zilitolewa na wana-Mtwara, CUF Taifa haikuwa na msaada wowote” alisema Abdallah.

Abdallah alijiunga na CUF mwaka 2000 katika tawi la Chemchem, Kinondoni, mkoani Dar es Salaam . Alihamia tawi la Mzambarauni, kata ya Likombe, wilaya ya Mtwara mjini mwaka 2010 na kupata nafasi ya kugombea ubunge jimbo la Mtwara mjini kupitia tiketi ya chama hicho.

Mwisho