WACHOMA MOTO JENEZA

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida waumini wa dini ya Kiislamu katika kijiji cha Nyundo B, Kata ya Nitekela halmashauri ya wilaya ya Mtwara wamelivunjavunja Jeneza na kisha kulichoma moto muda mfupi baada ya kutumika kumzikia mwanakijiji mwenzao ambaye alikuwa muumini wa dini ya Kikristo.

Tukio hilo limetokea Februari, 24 mwaka huu saa nane mchana na kuzua mjadala kijijini hapo, huku kundi hilo la waislamu wakidai ni bidaah (haramu) kwa Janeza linalotumika kuzikia Waislamu kutumika kwa watu ambao sio Waislamu.

Kaimu Mtendaji wa Kijiji hicho, Saidi Chitale ameiambia KUSINI kuwa siku moja kabla ya tukio, mwanakijiji mwenzao aliyemtaja kwa jina la Leonado Pius (72) ambaye ni muumini wa dini ya kikristo alifakiri na kuzikwa siku ya pili yake ambapo viongozi wa dini hiyo walikwenda msikitini kuazima Jeneza kwa ajili ya kwenda kumzika marehemu.

Alisema kuwa Mwenyekiti wa Kigango cha Nyundo B, Benedict Namadengwa alikwenda kwa sheikh mkuu wa kijiji hicho Seleman Mussa  kuazima Jeneza hilo na kuruhusiwa kwa sharti la kulirejesha msikitini hapo mara baada ya kukamilika kwa shughuli za mazishi.

“Baada ya mazishi Jeneza lilirudishwa Msikitini ambako walilichukua, cha ajabu baadaye kundi la wasilamu walifika msikitini hapo na kulitoa Jeneza nje na kuanza kulivunjavunja, walilimwagia mafuta ya Petroli na kulichoma moto…wanadai kitendo kilichofanyika ni bidaah” alisema Chitale

Sheikhe Mussa alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo, alithibitisha kutokea na kuongeza kuwa kitendo kilichofanywa na waumini hao si chema na hakina budi kulaaniwa.

“Jeneza limetengenezwa kwa ajili ya kubeba maiti na kupeleka mazishini, hakuna matumizi mengine zaidi ya hayo…hakuna bidaah (haramu) yoyote ile kwa Jeneza linalotumiwa na Waislamu likitumiwa na asiye muislamu” alisema Sheikhe Mussa ambaye pia ni Imamu wa Msikiti huo.

Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Hamisi Adinan alisema hakuna kosa lolote kwa upende wa imani kwa Jeneza linalotumiwa na Waislamu likitumiwa na Wakristo na kusema kuwa waliotenda kitendo hicho wamekwenda kinyume na maamrisho ya Mungu.

“Hakuna kosa lolote, kwa Jeneza la Waislamu  kubeba mwili wa Mkristo…nimesikitishwa sana na kitendo kilichofanywa na waislamu hao…tusifike huko, tusome maandiko yanasemaje, hakuna inapoharamishwa hilo” alisema Sheikhe Adinani

Baadhi ya wanakijiji wameelezea kusikitishwa kwao na kitendo hicho kwa madi kinaonesha unyanyasaji kwa mwili wa marehemu na familia iliyobaki.

“Utafikiri aliyezikwa si binadamu mwezao…ni jambo ambalo sisi kama wanakijiji linatuumiza sana kwa sababu linatujengea mahusiano mabaya baina ya dini hizi mbili” alisema John James mkazi wa kijiji hicho

Mwisho