CARE INTERNATIONAL KUWAGA PESA KWA WANAWAKE KUSIN​I

Ofisa Jinsia na Utawala bora wa shirika la Care International, mkoani Mtwara Getruda Phinias akimwelekeza jambo mgeni rasmi wa siku ya Wanawake Duniani katika halmashauri ya Mtwara, Mohemedi Livanga ambaye ni diwani wa kata ya Mtiniko (kushoto) Picha na KuSINI

SHIRIKA la Care International limezindua mradi wa miaka Mitano wa kuwawezesha kiuchumi wanawake na watoto wa mikoa ya kusini Lindi na Mtwara, ulioanza kutekelezwa mapema mwezi huu.

Ofisa Jinsia na Utawala bora wa shirika hilo, mkoani Mtwara Getruda Phinias alisema awali Care ilikuwa inajishughulisha na kusaidia wakimbili na kwamba kwa sasa shirika hilo la kimataifa linajishughulisha na maendeleo.

Akitoa taarifa katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Ndumbwe halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Phinias alisema kuwa asasi hiyo inawawezesha wanawake katika masuala ya kilimo, ususi na ushonaji ili kuwakomboa kiuchumi.

“Care imebaini kuwa wanawake wengi wamekuwa wakinyanyaswa na wanaume kwa sababu ya hali zao za utegemezi, hawana kipato…hali hii inawafanya waendelee kuwa wanyonge” alisema ofisa huyo.

Aliongeza kuwa “Katika kukabiliana na hali hiyo, tumeamua kuwewawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwaunga mkono katika katika shughuli za kuwaingizia kipato iwamo usindikaji wa muhogo, kilimo cha ufuta, ususi na ushonaji”

Alifafanua kuwa mradi huo wa miaka mitano utatekelezwa katika wilaya za Masasi na halmashauri ya Mtwara kwa mkoa wa Mtwara na wilaya za Ruangwa na Lindi kwa mkoa wa Lindi.

Diwani wa kata ya Mtiniko, halmashauri ya wilaya ya Mtwara, Mohamedi Livanga ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo aliwataka wanawake kukataa hali ya kunyanyaswa na wanaume kwa kujiimarisha kiuchumi.

“Ukiwa una fedha, mali hakuna mwanaume atakaye kubabaisha, wanaume watakunyenyekea na kukuheshimu…lakini kama huna kitu hata kama tutaendelea kulalamika kila siku bado wanaume wataendelea kuwanyanyasa kwa sababu ya umasikini wenu” alisema Livanga.

Mwisho.