POLISI MTWARA YAMDHIBITI MBATIA

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi James Mbatia akisisitiza jambo katika moja ya mikutano yake mjini Mtwara

SIKU ya Jumapili ilikuwa siku hasi kwa chama cha NCCR Mageuzi baada ya polisi kukinyima kibali cha kuaandamana kushinikiza Serikali kuwalipa fedha zao wakulima wa korosho, kupinga kupelekewa gesi jijini Dar es Salaam kabla ya kunufaisha wakazi wa mkoa wa Mtwara ambapo katika hatua nyingine mkutano wao wa adhara ulishindwa kufana baada ya mvua kunyesha na kuathiri maudhurio.

Chama hicho mapema wiki iliyopita kilitangaza kuwa juzi Jumapili kingefanya maandamano makubwa ya amani ya kufikisha vilio vya wananchi wa Mtwara kwa Serikali yao , maandamano ambayo yangeishia kwa kufanyika kwa mkutano mkubwa wa adhara katika viwanja vya Mashujaa mjini hapa.

Mbali na kutofanyika kwa maandamano hayo, pia mkutano wa adhara ulishindwa kufana baada ya mvua kuendelea kunyesha hali iliyoathiri maudhurio, hata hivyo mwenyekiti wa chama hicho James Mbatia alizungumza na wananchi wachache waliozingira jukwaa kuu.

Mvua ilianza kunyesha mapema saa 8 mchana na kuendelea hadi saa 12 jioni hali iliyosababisha watu wengi kushindwa kuudhuria mkutano huo ambao Mbatia aliutumia kuwaaga wana-Mtwara na kuwashukuru kwa kukiunga mkono chama chake.

Kabla ya Mbatia kuzungumza, Katibu Mwenezi wa chama hicho Taifa, Moses Machali aliiambia hadhira hiyo kuwa maandamano yameshindwa kufanyika baada ya polisi kukataa kutoa kibali kwa sababu ya mgomo wa madaktari.

“Naomba polisi wajisahihishe, hakuna uhusiano wowote kati ya mgomo wa Madaktari (Umekwisha kwa sasa) na maandamano ya Mtwara…NCCR-Mageuzi wapo waliosoma, wenye uwezo wa kuchanganua mambo, hii sio sababu ya msingi ila tumetumia busara kuliacha hilo , wakati mwingine hatutakubali sababu dhaifu kama hizo” alisema Machali ambaye pia ni Mbunge wa Kasulu  

Aliongeza kuwa “Polisi wanapaswa kujiepusha na utendaji kazi wa kuzingatia maagizo ya CCM, sisi tulitaka kupaza sauti za wanyonge wa Mtwara ambao hadi sasa fedha zao za mauzo ya korosho hawajalipwa, na rasilimali yao ya gesi inataka kupelekwa Dar es Salaam kabla ya kuwanufaisha wenyewe”

Akihutubia wananchi hao, Mbatia alisema amesikitishwa sana na kitendo cha polisi kuzima maandamano yao ya amani na kutoa wito kwa jeshi hilo kuheshimu msingi ya Katiba na kuepuka kufanya kazi zake kwa kukipendelea chama kimoja.

“Sisi bendera yetu ina alama nyeupe, hii inaashiria kuwa sisi ni watu wa amani, mukiendelea kuleta ufyoko ufyoko tutawajibu…mgomo wa madaktari na kutembea kwetu Mtwara wapi na wapi, huu wendawazimu” alisema Mbatia akikosoa hoja za polisi za kuwanyima kibali cha kuandamana.

Alisisitiza kuwa “Kupitia wakuu wa wilaya na mikoa, yote dola yote inakuwa makada wa CCM, kinyume na Katiba ya nchi inayotamka wazi kuwa vyombo vya dola, vikiwemo, Polisi, Wanajeshi, JKT, Magereza na vyombo vingine sio wanachama wa chama chochote cha siasa…ndugu zangu katika mchakato wa katiba mpya tushauri dola iwe inajitegemea”

Akizungumzia ziara yake ya siku nane mkoani Mtwara Mbatia alikosoa uwamuzi wa Serikali wa kuwapatia sehemu ya Bandari ya Mtwara wawekezaji wa gesi na mafuta, na badala yake aliishauri serikali kuwapatia eneo ili wajenge bandari ya kwao kulingana na mahitaji yao .

“Wao ni wawekezaji matajiri, kwanini wasipewe eneo ili wajenge bandari ya kwao, unapowapa eneo ndani ya banadari tuliyorithi kwa wakoloni, kesho utasikia bandari imebinafsishwa” alisema Mbatia

Aliongeza kuwa “Serikali kabla ya kujenga Bandari ya Bagamoyo ilipaswa kuimarisha Bandari za Mtwara, Dar es Salaam na Tanga, unawezaje kuanza mradi mwingine wakati huu ulionao haujaimarika…zipo wapi meli za abiria Mtwara? alihoji

Mbatia aliahidi kurudi mkoani Mtwara Mei, mwaka huu ili kuendelea na mikutano ya kukijenga na kukiimarisha chama chake ambacho alijigamba kuwa kimeonesha mafaniko makubwa mkoani humo

Mwisho

Advertisements