MTWARA HATARINI KUKOSA MAJI

 

Mashamba katika Bonde la Mtawanya ambako kuna vyanzo vya maji vinavyolisha Manispaa ya Mtwara-Mikindani

MANISPAA ya Mtwara-Mikindani ipo hatarini kukosa huduma ya maji baada ya wananchi kuvamia na kuendesha shughuli za kilimo maeneo ya chanzo cha maji cha Mtawanya ambacho kinalisha mji huo.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Ofisa wa Maji wa Bonde la Mto Ruvuma na Pwani ya kusini, Razalo Msaru alipokuwa akiongea na KUSINII ofisini kwake ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya maji.

Alisema bonde la Mtawanya ambalo kwa sasa lina visima vya maji 10 limevamiwa na wananchi kwa kuendesha shughuli za kilimo hali ambayo alisema inaweza kusababisha kukauka kwa visima hivyo.

“Bonde la Mtawanya lina visima 10, kati ya hivyo Saba ndivyo vinavyozalisha maji …changamoto kubwa inayotukabili katika uendeshaji wa visima hivyo ni uvamizi wa wananchi wa maeneo hayo katika bonde hilo, wanaendesha shughuli za kilimo” alisema Msaru

Alifafanua kuwa “Vyanzo hivyo Saba vinazalisha lita 7.5 milioni kwa siku wakati mahitaji ni lita 12 milioni, maji tunayoyapata hayatoshi hivyo iwapo wananchi wataendelea na tabia ya kulima katika lile bonde, wanaweza kusababisha kadhia kubwa ya kukosa maji kwa wakazi wa Mtwara…zaidi ya asilimia 80 ya maji ya Mtwara yanatoka Mtawanya”

Alieleza kuwa ofisi yake imeanza kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo kwa kuanzisha vikundi vya watumia maji katika vijiji vyote 10 vinavyolizunguka bonde hilo.

“Kupitia vikundi hivyo wananchi wanaelimishwa juu ya umuhimu wa utunzaji wa maji…maji yakikauka hayana mbadala…tofauti na kilimo kwani wanaweza kwenda kulima kokote mbali na bonde hilo” alisisitiza ofisa huyo.

Alibainisha kuwa vikundi hivyo vitaunda jumuiya ya watumiaji maji ambayo itahusika na utunzaji shirikishi wa vyanzo hivyo vya maji.

“Wakati hilo likiendelea tumeamua kuweka vibao vya kuwataadhirisha wananchi kuacha tabia ya kuendesha shughuli za kilimo katika bonde la Mtawanya” alisema Msaru

Mwisho

 

 

Advertisements