BEI YA SAMAKI MTWARA KUSHUKA

Mratibu wa Umoja wa Wafugaji Samaki Mtwara,(Uwasa) ,Hadija Malibiche akimkabidhi baiskeli mwenyekiti wa Umoja wa Wafugaji wa Samaki Mtwara (Uwasa), Masoudi Kuota, hafla hiyo ilifanyika jana mjini Mtwara.

BEI ya Samaki mkoani Mtwara inatarajia kushuka mara dufu katika kipindi cha mwezi mmoja ujao na kuwawezesha wakazi wake kumudu kutumia kitoweo hicho kwa mahitaji ya chakula.

Hayo yamebainishwa jana na Mratibu wa Umoja wa Wafugaji Samaki Mtwara,(Uwasa) ,Hadija Malibiche katika hafla fupi ya kukabidhi baiskeli Sita zenye thamani ya sh. 720,000 zilizotolewa na shirika la misaada la Swiss Aid Tanzania kwa wasimamizi wa mabwawa.

Alisema umoja huo unatarajia kuvuna zaidi ya tani 10 za samaki kuanzia Aprili mwaka huu kutoka kwenye mabwawa Sita yaliyopo Mtwara vijijini.

“Sote tunafahamu kuwa bei ya samaki kwa sasa mkoani Mtwara ipo juu sana, huwezi kufikiri kirahisi kuwa Bahari ipo pembeni yetu, Samaki tunaouziwa hawana thamani ya fedha tunayolipa ila tunalazimika kununua ili kukidhi mahitaji yetu” alisema Malibiche

Mratibu wa Uwasa akiwa katika picha ya pamoja na wasimamizi wa mabwawa

Aliongeza kuwa “Moja ya sababu ya kupanda kwa bei ya Samaki Mtwara ni wavuvi kutumia zana duni za uvuvi hivyo kusababisha kuvua Samaki wachache ili hali mahitaji ni mengi…Umoja wetu unataraji kushusha bei za Samaki kwa kuingiza sokoni zaidi ya tani kumi za Samaki kuanzia Aprili mwaka huu”

Alibainisha kuwa mbali ya samaki hao kuwainua wanachama wa vikundi hivyo kiuchumi, pia watasaidia wakazi wa mkoa huo na maeneo jirani kuweza kumudu kununua kitoweo hicho.

Alisisitiza kuwa msaada wa baiskeli kwa wasimamizi wa mabwawa unalenga kuboresha shughuli za ufugaji ili lengo la mavuno liweze kutimia.

Mratibu wa Uwasa akimkabidhi baiskeli katibu wa umoja huo Mvita Shona

“Uwasa ni muungano wa vikundi vidogo vidogo 14 vya wafugaji wa Samaki kutoka kwenye vijiji Sita  vya Mbuo, Ndumbwe, Kisiwa, Namgogoli, Msimbati na Mindondi…Umoja huu unajishughulisha na ufugaji wa samaki na utunzaji wa mazingira” alisema Malibiche

Mwenyekiti wa Uwasa, Masoudi Kuota aliishukuru Swiss Aid kwa msaada wa baiskeli hizo na kuongeza kuwa zitarahisisha kazi kwa wasimamizi wa mabwawa kuyazungukila na kutoa ushauri wa kitaalam.

“Ilikuwa vigumu kwao kuzungukia mabwawa yote kutokana na kukosa usafiri, lakini sasa kazi ya usimamizi itakwenda vizuri, naishukuru sana Swiss Aid’ alisema Kuota.

Mwisho

Advertisements