OFISI YA OCD, VIBANDA VYA BAISHARA ZAIDI YA 50 VYATEKETEZWA KWA MOTO

OFISI ya mkuu wa polisi wa wilaya ya Tandahimba, (OCD) mkoani Mtwara na vibanda vya biashara zaidi ya 50 vimeteketea kwa moto baada ya watu wasiojulikana kuchoma moto na kusababisha harasa ya mamilioni ya shilingi.

Tukio hilo limetokea jana saa 3: usiku ambapo habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa ofisi ya OCD ndiyo iliyoanza kuwaka moto kabla ya kudakia vibanda vya biashara ambavyo hadi kufikia saa 2 asubuhi vilikuwa vinaendelea kuwaka moto.

Ofisi hiyo ya OCD ipo eneo la soko kuu la mjini Tandahimba mita 200 kutoka kituo kikuu cha polisi cha wilaya na imezungukwa na vibanda vya biashara ya maduka ya nguo, vifaa vya ujenzi na bidhaa mbalimbali.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Focus Malengo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa hadi sasa watu 52 wanashikiliwa na jeshi lake kwa uchunguzi zaidi.

“Ofisi ya OCD na vibanda vya biashara zaidi ya 50 vimeteketea kwa moto…bado thamani ya mali zilizoteketea haijajulikana hadi sasa…nyaraka zote zilizokuwamo ofisini humo zimeteketea, tunawashikilia watu 52 kwa uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo” alisema Malengo

Alifafanua kuwa “Chanzo cha tukio hilo halijajulikana, tunaendelea na uchunguzi ili tuweze kubaini sababisho la moto huo…tunajaribu kuangalia kama tukio hilo linauhusiano la madai ya wakulima, siasa au chuki dhidi ya jeshi la polisi na serikali”

Habari kutoka eneo la tukio zinadai kuwa jeshi la polisi lilirindimisha mabomu ya machozi mfululizo kuanzia saa 3 usiku huo hadi saa 12 asubuhi na kusababisha watu kuyakimbia makazi yao na kwenda kusikojulikana.

Uchunguzi ulifanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa nyumba nyingi za wakazi wa katikati ya mji wa Tandahimba na mitaa yake ikiwa tupu huku ikielezwa kuwa vijana wa kike na wakiume wamekimbilia mapolini kuhofia usalama wao.

Kamanda Malengo alisema hakuna polisi wala raia aliyeripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo na kuongeza kuwa Kamishina  wa Operesheni wa Polisi CP, Paul Chagonja anatarajia kuwasili wilayani humo jana (leo) kwa Helkopta kujionea hali halisi.

Aidha Kamanda Malengo amesema jumla ya watu tisa kati ya watu zaidi ya 50 waliokamatwa katika tukio lililotokea mwishoni mwa wiki wamefikishwa Mahakamani na wengine wameachiwa huku uchunguzi ukiendelea ili kubaini kama wanahusika na tukio hilo.

Vurugu wilayani Tandahimba zilianza Aprili 12 siku moja baada ya wakulima wa korosho kuandamana kuishinikiza serikali kuwalipa malipo ya pili ya mauzo ya korosho zao, ambapo polisi alijeruhiwa, miundombinu ya barabara, maji na umeme viliharibiwa huku barabara za kuingia na kutoka wailayani humo zikifungwa kwa magogo na miti mikubwa.

Hata hivyo jeshi la Polisi limesema hawana ushahidi wa moja kwa moja wa kuhusianisha tukio la jana na vurugu za wakulima na kwamba wanaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo na uhusiano uliopo kati ya matukio hayo mawili.

Mwisho

Advertisements