POLISI WADAIWA KUCHOMA MABANDA TANDAHIMBA

Mabanda yaliyoteketezwa kwa moto mjini Tandahimbab

WAFANYABIASHARA hambao vibanda vyao vimeteketea kwa moto juzi usiku wilayani Tandahimba, mkoani Mtwara wamedai kuwa polisi walipora mali za dukani na kuwazuia wananchi kuzima moto kwa kuwapiga mara walipojaribu kukaribia eneo hilo.

Wafanyabishara hao walimweleza hayo Kamishina wa Opareshenin wa jeshi la polisi, Paul Chagonja mjini Tandahimba jana mara alipotembelea eneo la tukio na kujionea hali halisi.

Kamanda Chagonja ambaye aliongozana na maofisa wengine wa polisi alilakiwa na kundi la wananchi ambao mara alipotaka kuondoka walimuomba wamueleze kile walichodai ndiyo ukweli wa tukio hilo

Mabanda yaliyoteketea

“Polisi waliingia dukani na kupora simu, walikuwa wanagawana huku tunawaona…wakija mbele yetu tunaweza kuwatambua bila shaka” alisema Shabuki Ulenje mmiliki wa moja ya mabanda yaliyoungua.

Aliongeza kuwa “Kila tulipojaribu kwenda eneo la tukio ili tuweze kuzima moto kunusuru mali zetu polisi walituzuia kwa kutupiga…kama sio wao kutuzuia moto usingeteketeza kwa kiwango hiki”

Mfanyabiashara mwingine Ahmadi Ismail pia aliunga mkono maelezo ya mwenzie na kuongeza kuwa polisi walikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio ambapo badala ya kutoa msaada walivamia maduka na kupora mali.

Mkazi mwingine ambaye ni mwendesha pikipiki eneo la kituo kikuu cha mabasi, aliyejitambulisha kwa jina moja la Mandisa alimwambia Chagonja kuwa alikuwa miongoni mwa watu waliopigwa na polisi pale alipojaribu kwenda eneo la tukio kutoa msaada.

Escudo ni miongoni mwa vitu vilivyoteketea katika tukio hilo

“Mimi nimepigwa kama unavyoniona, askari mmoja wa Mtwara ndiye aliyenipiga zaidi, wakiletwa mbele yangu naweza kumjua…nilikuwa nakwenda kusaidia kuzima moto” alisema Mandisa

Baada ya kusikiliza kilio hicho cha wananchi, Chagonja alionesha kutaka kukwepa kujibu hoja hizo za wananchi hadi pale waandishi wa habari walipomtaka kutolea majibu.

“Kama wapo askari waliohusika na vitendo hivyo hao hatutawaacha…tutawashughulikia, kama nilivyosema awali cha msingi tunakwenda kufanya uchunguzi na hili tutalichunguza” alisema Chagonja

Aidha alieleza kuwa watu 52 walioshikiliwa ka madai ya kuhusiaka na tukio hilo wameachiwa kwa dhamana wakati uchunguzi ukiendelea na kwamba watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua za kisheria.

“Tunajua hata kama kuna watu wanaohusika basi sio wote, tutafanya uchunguzi wa kitaalam ili kuwabaini na kisha kuwafikisha Mahakamani…kuna watu wanajinufaisha na hizi vurugu ndiyo maana wanaazisha” alibainisha kamanda huyo

Watu wasiojulikana juzi usiku walichoma moto ofisi ya  mkuu wa polisi wa wilaya ya Tandahimba, (OCD) mkoani Mtwara na vibanda vya biashara zaidi ya 50 vimeteketea kwa moto baada ya watu wasiojulikana kuchoma moto.

Kufuatia hali hiyo Kamishina wa Polisi wa Operesheni CP, Chagonja aliwasili wilayani humo kujionea hali halisi baada ya kuwapo kwa matukio mfululizo ya uvunjifu wa amani katika kipindi cha wiki moja sasa.

Vurugu wilayani Tandahimba zilianza Aprili 12 siku moja baada ya wakulima wa korosho kuandamana kuishinikiza serikali kuwalipa malipo ya pili ya mauzo ya korosho zao, ambapo polisi alijeruhiwa, miundombinu ya barabara, maji na umeme viliharibiwa huku barabara za kuingia na kutoka wailayani humo zikifungwa kwa magogo na miti mikubwa.

Wakati hayo yakitokea Polisi mkoani Mtwara kupitia kwa Kaimu Kamanda wake Focas Malengo limesema linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha tukio hilo.

“Hadi sasa hatuna ushahidi wa moja kwa moja  kuhusianisha tukio la juzi na vurugu za …tunaendelea na uchunguzi”alisema Malengo

Mwisho

 

Advertisements