LIPUMBA APOKEWA KWA VILIO TANDAHIMBA

Pro. Ibrahim Lipumba akimfariji Abdallah Abdallah mmoja wa wafanyabisha ambae anadai kuwa gari yake ilichomwa moto na polisi

WAFANYABIASHARA wa wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara ambao mabanda yao yameteketea kwa moto Aprili 17, mwaka huu, mwishoni mwa wiki walimpokea Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF)Taifa  Pro. Ibrahim Lipumba kwa vilio alipotembelea eneo la tukio kuona hali halisi.

Lipumba akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wake, Julius Mtatilo aliwasili wilayani humo Aprili, 21 mwaka huu na kulakiwa na wafanyabishara ambao wengi wao walikuwa wakimbumbujikwa na machozi.

Akiwa katika eneo la tukio Lipumba alipata maelezo kutoka kwa wafanyabishara hao ya namna moto huo ulivyozuka na jinsi jitihada za kunusuru mali zao zilizvyogonga mwamba na hivyo kusababisha mali zenye thamani ya mamilioni ya shilingi kuteketea.

Akiongea huku machozi yakimdondoka, mfanyabishara Abdallah Abdallah ambaye gari na kibanda chake cha biashara vimetetea kwa moto huo alidai kuwa moto huo umesababishwa na baadhi ya polisi.

Alisema yapata saa 2:30 usiku alipigiwa simu na mdogo wake anayeuza duka lake katika eneo la sokoni na kuarifiwa juu ya kuzuka kwa moto katika ofisi ya mkuu wa polisi wawilaya hiyo.

Alidai kuwa alipofika katika eneo hilo huku akiwa anaendesha gari lake Escudo T323 AQV, ghafla alisimamishwa na polisi waliovalia sare huku wakiwa wamebeba silaha na baada ya mahojiano walimwamru ateremke ndani ya gari na kutokomea.

 

“Nilisimamishwa na askari …(alimtaja jina), aliamru nizime taa, kikazima, nikajitambulisha kwao na kuwaambia kusudi langu la kuja katika eneo hilo….ghafla nilishtuka kuona askari wakipasua tairi ya nyuma ya gari langu kwa kupiga risasi, mara mwingine akaja na kupasua

kioo upande wa wangu kwa kutumia panga” alidai Abdallah

Wakazi wa Tandahimba, mkoani Mtwara wakiangalia mabaki ya mabanda yaliyotoketea kwa moto hivi karibuni ambapo ofisi ya mkuu wa polisi wa wilaya hiyo pia iliteketea

 

Wakazi wa Tandahimba, wakiangalia mabaki ya gari inayodaiwa kuchomwa moto na polisi

Aliongeza kuwa “Wakati huo moto ulikuwa haujafika hata kwenye kibanda kimoja… nikaambiwa nitoke la sivyo watanimaliza, nilitoka na kwenda kujificha, walianza kuiponda ponda na baadaye walifuata petroli na kuichoma moto…amani hii ni ya watu wachache, walioshika dola”

Mfanyabishara mwingine aliyedondosha machozi mbele yake ni Hamisi Mandisa mwendesha pikipiki eneo la kituo kikuu cha mabasi,  aliyedai kuwa alipigwa na pikipiki yake kuchomwa moto na askari polisi.

“Walinisimamisha, niliposimama askari mmoja alikuja na kuanza kupiga, ‘konfuu’ moja ya shingo (ngumi) ananipiga tena nikaanguka chini, wakaniambia kimbia wasije kunimaliza…nikambia na kuacha pikipiki, sikuwa na wasiwasi na pikipiki kwa sababu kati ya hao askari alikuwapo mmoja ninayefahamisha vizuri , lakini asubuhi nilipofika eneo la tukio nilikuta imechomwa moto” alieleza Mandisa huku akiangukwa na machozi

Wakati wafanyabishara hao na wengine walipokuwa wakitoa maelezo wengine walikuwa wamegubikwa na sura za uzuni na vilio vya kwikwi vilisikika kutoka miongoni mwao.

Mwendesha pikipiki Hamis Mandisa mkazi wa wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara alimweleza mwenyekiti wa CUF Taifa Pro. Ibrahim Lipumba (Hayupo pichani) jinsi alivyochomewa moto pikipiki yake na kisha mwenyewe kupigwa na polisi

Baada ya kusikiliza maelezo kutoka kwa wafanyabishara zaidi ya 15 Lipumba aliwapa pole na kuwataka kuwa wavumilivu katika kipindi hicho kigumu, huku akisema kuwa tukio hilo limezingirwa na utata.

“Miaka 50 ya uhuru bado wapo polisi wanaodhulumu na kutesa raia…ni aheri polisi wa kikoloni walikuwa na huruma kuliko hawa…nimesikia nitaangalia uwezekano wa kuwasaidia mwanasheria ili kuangalia uwezekano wa kufungua kesi ya madai” alisema Lipumba

Aliongeza kuwa “Ushari wangu kwenu andikeni maelezo hayo ili muwe na kumbukumbu sahihi, musiongeze wala kupunguza, andikeni uwkeli tupu…kama hilo ngumu basi mujirekodi”

Kamishina wa oparesheni wa polisi Paul Chagonja mara alipopokea maelezo kama hayo ya wafanyabishara aliahidi kulifanyia kazi na wanataobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

“Kama wapo askari waliohusika na vitendo hivyo hao hatutawaacha…tutawashughulikia, kama nilivyosema awali cha msingi tunakwenda kufanya uchunguzi na hili tutalichunguza” alisema Chagonja

Aliongeza kuwa  “Tunajua hata kama kuna watu wanaohusika basi sio wote, tutafanya uchunguzi wa kitaalam ili kuwabaini na kisha kuwafikisha Mahakamani…kuna watu wanajinufaisha na hizi vurugu ndiyo maana wanaazisha” alibainisha kamanda huyo

Watu wasiojulikana juzi usiku walichoma moto ofisi ya  mkuu wa polisi wa wilaya ya Tandahimba, (OCD) mkoani Mtwara na vibanda vya biashara zaidi ya 50 vimeteketea kwa moto baada ya watu wasiojulikana kuchoma moto.

Kufuatia hali hiyo Kamishina wa Polisi wa Operesheni CP, Chagonja aliwasili wilayani humo kujionea hali halisi baada ya kuwapo kwa matukio mfululizo ya uvunjifu wa amani katika kipindi cha wiki moja sasa.

Mwenyekitiwa CUF taifa Pro. Ibrahim Lipumba akisisitiza jambo alipokuwa nawapa pole wafanyabishara wa wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara ambao vibanda vyao vya baishara vimeteketea kwa moto wiki iliyopita.

Vurugu wilayani Tandahimba zilianza Aprili 12 siku moja baada ya wakulima wa korosho kuandamana kuishinikiza serikali kuwalipa malipo ya pili ya mauzo ya korosho zao, ambapo polisi alijeruhiwa, miundombinu ya barabara, maji na umeme viliharibiwa huku barabara za kuingia na kutoka wailayani humo zikifungwa kwa magogo na miti mikubwa.

Mwisho

 

Advertisements