HATUJAUZA BANDARI YA MTWARA-SERIKALI

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba akisisitiza jambo

SERIKALI imekanusha habari kuwa Bandari ya Mtwara imeuzwa kwa kampuni za kigeni zinazofanya utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi mkoani humo.

Naibu Waziri wa Uchukuzi Injinia Charles Tizeba alisema hayo jana mjini Mtwara wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wiki mbili ya uendeshaji bora wa Pikipiki kwa waendesha Pikipiki 600 wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani yanayoendelea chuo cha ualimu ufundi mjini hapa.

Alisema kuwa habari zilizoenea hivi karibuni zinazodai kuwa serikali imeuza bandari ya Mtwara kwa wawekezaji si za ukweli na wala hakuna mpango wowote wa serikali wa kutaka kuiuza na kwamba bandari hiyo bado ni mali ya Watanzania.

“Yapo maneno kuwa bandari ya Mtwara imeuzwa, hata nyie mmesikia?” aliuliza Tizeba na kujibiwa waendesha Pikipiki “Ndiyooo” …. “Hizi tetesi za kuuzwa bandari naomba niwahakikishie Watanzania wenzangu kuwa haijauzwa” alikanusha naibu naziri huyo

Alifafanua kuwa “Wale watu tumewakodisha sehemu ya bandari, kwani mwenye nyumba akiamua vyumba vingine kupangisha ina maana umeiuza nyumba yake?… Bado nyumba inaendelea kuwa yake na siku mpangaji akishindwana nae anamtimua, ndicho tulichokifanya…sisi tupo macho”

Alisema kuwa Serikali ililazimika kuwakodisha sehemu ya bandari hiyo kutokana na shughuli za makampuni hayo ya utafiti na uchimbaji wa gesi na mafuta baharini kuhitaji eneo la bandari ili waweze kuendesha shughuli zao.

Tizeba ambaye alitumia muda mrefu kukanusha hoja hiyo alisema “Si bandari ya Mtwara, Dar es Salaam au Tanga iliyouzwa kwa mwekezaji yoyote…iwapo serikali itaamua kuuza, mutajua, itatangazwa … hadi sasa hakuna bandari iliyotangazwa kuuzwa”

Akizungumzia mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na kampuni ya Utafiti wa Mafuta na Gesi baharini ya BG Tanzania, naibu waziri huyo alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu na mali.

“Nawapongeza BG Tanzania kwa kufadhili mafunzo haya ambayo yataongeza chachu ya usalama barabarani na kupunguza ajali…Nawapongeza askari wa usalama barabarani kwa kusimamia vema kazi yao, nilipofika hapa nimeona kila mwendesha pikipiki amevaa kofia yeye na abiria wake…maeneo mengine pia yaige Mtwara” alisema Tizeba

Awali Kamishina wa usalama barabarani nchini, Mohamedi Mpingu alisema mafunzo hayo yanayoendehswa na chuo cha usafirishaji nchini ni ya kwanza kutolewa kwa waendesha Pikipiki hivyo kuagiza mikoa mingine kuiga mfano wa Mtwara ili kuepusha ajali za barabarani zinazosababishwa na vyombo hivyo vya usafirishaji abiria.

“Ukienda hospitali za mikoa utakuta wadi zimeandikwa “sunlg”, hii ina maana tatizo la ajali za pikipiki ni kubwa kiasi hospitalini watenge wadi maalum kwa ajili yao…hili linalofanyika leo hapa ni jambo muhimu kwa usalama barabarani, naomba mikoa mingine iige kutoka Mtwara” alisema Kamanda Mpingu

Aliongeza kuwa “Pamoja na takwimu kuonesha kuwa ajali za Pikipiki zimepungua nchini, lakini bado tunatakiwa kuongeza kasi ya kupambana nazo, njia muhimu hapa ni kutoa elimu kwa waendeshaji wa vyombo hivyo… sisi tunataka ukitoka asubuhi nyumbani basi urudi jioni ukiwa salama”

Mwakilishi wa BG Tanzania katika hafla hiyo, Emil Karuranga alisema kampuni yake iliamua kutoa kiasi cha sh. 72 milioni kufadhili mafunzo hayo ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwa jamii ya Mtwara ambayo kampuni hiyo inaendesha shughuli zake

Waendesha pikipiki wa manispaa ya Mtwara-Mikindani wakisikiliza wakati wa mafunzo yao

.

Michael Milale ni mwendesha Pikipiki anayehudhuria mafunzo hayo alisema licha ya kupunguza hatari ya kupata ajali lakini pia yataondoa migongano ya kiutendaj baina yao na askari wa usalama barabarani kwa kuwa watakuwa wanaelewa sheria na kanuni za usalama barabarani.

Mwisho

Advertisements