MADIWANI MASASI WAMKALIA KOONI OFISA UTUMISHI

MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara wamempa siku tatu ofisa utumishi wa halmashauri hiyo Lawrance Mhelela awe amewasilisha vyeti vyake vya taaluma ili mamlaka inayohusika ivihakiki baada ya kutilia shaka utendaji kazi wa ofisa huyo kuwa hauakisi taaluma yake.
Uwamuzi huo umefikiwa mwishoni mwa wiki katika kikao cha dharura cha baraza la madiwani hao, kilichoketi kwa lengo la kujadili mwenendo na utendaji kazi wa ofisa huyo, baada ya madiwani 26 kati ya 46 wa halmashauri hiyo kutia saini ya kutaka kuitishwa kwa kikao hicho.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jafari Mkwanda alikieleza kikao hicho kuwa madiwani hao waliwasilisha hoja hiyo kwake Mei, 25 mwaka huu kabla yeye kumwandikia barua mkurugenzi mtendaji Mei, 26 kwa ajili ya utekelezaji.
Alieleza kuwa wajumbe hao walibainisha hoja za kuitishwa kwa kikao hicho cha dharura kuwa ni pamoja na matumizi mabaya ya mali za halmashauri hiyo, kuajiri madereva wawili ambao licha ya kutokuwapo kwa magari ya kuendesha lakini pia ajira zao hazikufuata utaribu, kwenda kinyume na sheria ya manunuzi ya umma.
Hoja zingine ni pamoja na kutoudhuria vikao vya kiutendaji na anapoudhuria huonesha nidhamu mbovu, kupandisha vyeo watendaji wa vijiji kinyume na utaratibu, uzembe wa kutowasilisha nyaraka muhimu kwa wakati kwa ajili ya usajili wa vijiji na kushindwa kuwasimamia watumishi, hivyo kutokuwapo kwa uwajibikaji na kusababisha kuzorota kwa maendeleo ya halmashauri hiyo.
Baada ya mwenyekiti kufungua kikao hicho kwa kutoa utangulizi wa hoja zinazolalamikiwa na madiwani hao, kikao hicho cha baraza kilijigeuza kamati hali iliyosababisha waalikwa wakiwemo waandishi wa habari kutolewa nje ya ukumbi kabla ya kuitwa tena kwa ajili ya kuwalisha makubalinao yao.
“Baada ya kujadiliana haya na mengine mbalimbali, tumebaini kuwa vitendo hivyo vinaashiria kutokuwa na uwezo wa kitaaluma na hadhi ya kushika wadhifa huo…kamati imekubalina kuwa hadi kufikia Juma Tatu (leo) awe amewasilisha vyeti vyake vya taaluma kwa mkurugenzi mtendaji ili mamlaka zinazohusika wavihakiki” alisema Mkwanda
Alifafanua kuwa “Kama vyeti safi, tuhuma tulizozisema zishughulikiwe…kwa kipindi hiki mtuhimishi huyu atapumzika kufanya kazi hadi mambo mawili hapo juu yatakapokamilika”
Baada ya majadiliano yaliyodumu kwa zaidi ya saa mbili, kamati ilirudi kuwa baraza la madiwani na kupitisha maadhimio hayo yakiwemo ya kumpumuzisha ofisa huyo.
Akitolea ufafanuzi nje ya kikao mbele ya waandishi wa habari, mwenyekiti huyo alisema Mhelela anadaiwa kutumia Lori Isuzu lenye usajili namba SM 9721, mafuta na dereva wa halmashauri hiyo kwa kusomba mawe na mchanga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya makazi yake binafsi jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya matumizi ya mali za serikali.
“Mbali na hilo pia mtumishi huyu amekuwa akifanya biashara ya chakula na halmashauri kupitia mgahawa wake bila ya kufuata sheria ya manunuzi ya umma…pia alituhumiwa ku-supply nyama ya Nguruwe katika kikao cha baraza huku akijua si wote wanaotumia kitoweo hicho…tulimuonya lakini hakuonesha kujali” alisema mwenyekiti huyo
Aliongeza “Kama mulivyoona tulipowaita wajumbe tena, wakuu wengine wa idara walirudi lakini yeye hakurudi, na hii ndiyo tabia yake huwa haeshimu vikao na hata tunapoadhimia jambo na kulifikisha kwake kwa ajili ya utekelezaji huwa analipuuzia, tunawezaje kupata maendeleo kwa hali hiyo”
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Gladys Dyamvunye alisema hatua iliyochukuliwa na madiwani hao ni taratibu za kawaida za halmashauri za kushughulikia watumishi pindi wanawashtumu kwenda kinyume na utaratibu.
Kwa upande wake Mhelela alisema hadi kufikia Ijumaa iliyopita alikuwa hajapokea barua yoyote ya madai hayo ya madiwani hivyo hawezi kulizungumzia suala hilo hadi pale yatakapotua kwa maandishi mezani kwake.
“Sijapokea taarifa yoyote ya maandishi juu ya suala hilo, nitakapopokea basi nitajibu kwa mujibu wa hoja zitakazoletwa” alisema ofisa utumishi huyo anayeshtumiwa.
Mwisho

Advertisements