AJIFUNGUA CHINI YA MWEMBE AKIWA HOSPITALI, KICHANGA CHAFARIKI

Mbunge wa Newala George Mkuchika

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mjamzito mmoja amelazimika kujifungulia chini ya mwembe akiwa katika hospitali ya wilaya ya Newala mkoani Mtwara, na kusababisha kichanga kufariki dunia kutokana na huduma mbovu na lugha chafu zinazotolewa na wakunga wanawake hospitalini hapo.

Wakizungumza na KUSINI kwa nyakati tofauti katika wodi ya uzazi hospitalini hapo hivi karibuni wajawazito hao wamedai kuwa wamekuwa wakipewa huduma mbovu na lugha za matusi kutoka kwa wakunga pindi wanapoomba msaada.

Walisema katika tukio la hivi karibuni mama mmoja alifika hospitalini hapo kujifungua lakini alilazimishwa na mkunga aliyekuwepo zamu kwenda kufuata faili katika ofisi iliyokuwa mbali na alipojaribu kumuomba amsaidie alimtolea lugha kali za matusi na hivyo kulazimika kwenda kufuata faili hilo.

Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi

Walidai kuwa alipokuwa anafuata faili hilo alijifungulia chini ya mwembe na alipoomba msaada alichelewa kupata hali iliyosababisha kichanga chake kuanguakia katika mchanga na kufariki baadae.

Tukio la pili wakinamama hao walisema ni lililotokea hivi karibuni ambapo mama mmoja aliyekwenda kujifungua wodini hapo alichelewa kupata msaada na kusababisha mtoto wake kunywa uchafu hali iliyowalazimu madaktari kumchoma sindano 20 ili kunusuru maisha yake.

Grass Emilias mkazi wa kijiji cha Makong’onda ni mmoja kati ya kinamama waliokutwa na mwandishi wa habari hizi wodini akiuguza majeraha baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji, alisema licha ya matukio hayo lakini pia wamekuwa wakipewa lugha chafu na wakati mwingine kulazimishwa kufanya kazi ambazo zilitakiwa kufanywa na wakunga.

“Kwa mfano mama unafika hapa ukiwa taabani kabisa lakini wao watakwambia ujitandikie kitanda tena ufuate shuka kule kabatini…na ukishindwa basi utakumbana na maneno makali na unaweza kulala bila kutandika…lakini ukibahatika kuhudumiwa na mkunga wa kiume ni raha tupu tatizo ni hawa wenzetu wanawake”, alisema mama huyo.

Wakazi wa Newala mkoani Mtwara wakililia kupaza sauti zao kwa waziri mkuu wamueleze kero zao

Fatuma Imahili mkazi wa kijiji cha Makondeko, ambaye alijifungua kwa njia ya upasuaji na kupoteza mtoto wake, anaamini kuwa kama si uchelewashaji wa huduma angeweza kuwa na mwanaye lakini uzembe wa wakunga umesababisha mtoto kufariki muda mfupi baada ya kujifungua.

Mama mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mwajuma Rajabu mkazi wa Makonga mjini Newala, alisema kuwa kwa kipindi kirefu wodi hiyo imekuwa na matatizo makubwa ya utoaji wa huduma bora kwa wakinamama wanaokwenda kujifungua hasa wakunga wa kike ambao wanakuwa na lugha chafu na masimango dhidi yao.

Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dk. John Kamtande, anakiri kutokea kwa matukio ya kifo cha mtoto aliyeaangukia katika mchanga na lile la mtoto kunywa uchafu kutokana na kuchelewa kupata huduma lakini pia anakiri kupata malalamiko kutoka kwa wakinamama juu ya huduma zinazotolewa katika wodi hiyo.

“Ni kweli matukio hayo yapo na mimi nilikuwa safari nje ya wilaya kikazi nimerudi na nimepata taarifa juu ya matukio hayo…na nilipofika tu nimemwandikia barua mkunga muhusika ajieleze kama hatua ya awali ya kushughulikia tatizo hili”, alisema Kamtande.

Alisema tayari ameiarifu kamati inayohusika na malalamiko ya wateja dhidi ya watoa huduma na kwamba suala la mkunga aliyezembea wajibu wake hadi kusababisha kifo na yule aliyesababisha kichanga kunywa uchafu yanashughulikiwa na uamuzi uatatolewa baada ya kukamilika kwa uchunguzi unaoendelea.

“Ndugu mwandishi kimsingi hospitali yetu inatoa huduma nzuri kwa wateja na ndio maana tunapata wagonjwa wengi kutoka nje ya wilaya yetu…lakini kuna wenzetu wachache wanatuharibia sifa hii nzuri…unajua katika jumuiya kama hii ya watu wengi kunakuwa na wengine wenye tabia zisizo nzuri na wanafanya kazi kulinagana na tabia zao hili ni tatizo tunalishughulikia.

Naye mkunga mkuu wa hospitali hiyo, Regna Likwama, anasema kuwa ni kweli kumekuwa na malalamiko hayo lakini alisema wakati mwingine wanazidiwa na majukumu kutokana na uchache wao na ndio maana wamekuwa wanachelewa kutoa huduma.

“Unajua tupo wachache sasa mama mjamzito anapofika hapa anapoona hajahudumia kwa muda fulani wakati mkunga anamuhudumia mwingine yeye anaona kama anacheleweshwa makusudi…sio kusudio letu kuwanyanyasa wateja wetu…lakini pia nikiri tu kwamba kuna baadhi yetu wanakuwa sio waadilifu katika utendaji wa kazi” alisema Mkunga huyo mkuu.

Mwisho.

Advertisements