VIGOGO MTWARA WATAFUNA 12.32 MIL

VIGOGO wawili wa halmshauri ya wilaya ya Mtwara, mkoani hapa wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa wilaya hiyo, Agnes Futakamba wakituhumiwa ‘kutafuna’ milioni 12.32 za halmashauri hiyo zilizotolewa kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya makuzi ya mtoto.

Waliofikishwa mahakamni ni Hassan Seif Mwakipa ambaye ni ofisa tatibu msaidizi na Absolum Azaki Ntakandi ambaye mhasibu wafanyakazi wa halmshauri hiyo, hata hivyo Ntakandi hakuwepo mahakamani hapo.

Akiwasomea mashitaka 15 yanayowakabili mbele ya mahakama hiyo, mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (takukuru) Sospeter Tyeah alisema watuhumiwa wote wawili wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya tarehe 11hadi 16 Juni, 2009.

Alisema kuwa makosa hayo yamegawanyika katika maeneo matatu ambayo ni kula njama za kumdanganya mwajiri wao na kubadilisha matumizi ya fedha kwa manufaa yao binafsi, kugushi nyaraka na kuhujumu uchumi.

Tyeah alisema katika kosa la kwanza watuhumiwa wanadaiwa kutengeneza nyaraka za malipo ya jumla ya washiriki 25 wa mafunzo ya makuzi ya mtoto Juni 11, 2009 ambapo kila mmoja alilipwa 320,000,  wakati katika kosa la pili katika kipindi hicho watuhumiwa hao wanadaiwa kutumi karatasi zisizo na tarehe kuwalipa washiriki Saba 450,000 kila mmoja maelezo ambayo yamedaiwa kuwa ni ya uongo.

Mashtaka mengine ni pamoja na kumlipa Elizabeth Macha sh. 560,000  kuwa aliudhuria mafunzo hayo kama mwezeshaji, kuandaa risiti namba R07584 ya Januari, 4, 2010 ikieleza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo alimlipa Mkurugenzi wa Chuo cha Ushirika tawi la Mtwara sh. 129000 kama gharama za ukumbi.

Tyeah ambaye alitumia zaidi ya dakika 20 kusoma tuhuma hizo alidai kuwa watuhumiwa walitumia tiketi ya Ndege PW/MQQB7 ya Juni, 9, 2009 wakidai alitumia Elizaberth Macha kusafiria kwa ndege ya Presicion Air iliyogharimu sh. 368,000, pia risti isiyo na tarehe ikionesha mkurugenzi wa halmashauri hiyo alimlipa 750,000 mkuu wa chuo cha ushirika kwa ajili ya ukumbi.

Shtaka lingine ni pamoja na kuwapo kwa risti ya Juni, 12, 2009 ikionesha mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo amemlipa mtu ambaye hakutajwa kwa jina sh. 320,000 kununua karatasi kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo.

Mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru aliieleza mahakama kuwa watuhumiwa wanakabiliwa na mashtaka kama hayo ya kugushi nyaraka, kubadilisha matumizi ya fedha hizo na kuisababishia halmashauri hasara ya sh. 12.32milioni vitendo ambavyo pia ni makosa ya kuhujumu uchumi.

Mwendesha mashtaka huyo aliiomba mahakama kutoa dhamana kwa mtuhumiwa kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na sheria ambapo mtuhumiwa wa makosa ya kuhujumu uchumi kwa thamani inayozidi 10 milioni anatakiwa kulipa nusu ya fedha na kuwa na wadhamini wawili.

Mshtakiwa Mwakipa licha ya kukana makosa yote alirudishwa rumande hadi June, 25, mwaka huu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kutoa dhamana ya pesa taslimu sh. 6,160,000 na wadhamini wawili watakaomdhamini kwa sh. 3.5 milioni kila mmoja.

mwisho

 

 

 

 

 

 

 

Advertisements