‘UNGA’ WAUZWA NJE NJE MTWARA

Picha ya mkono wa mtu ikionesha anajidunga sindano ya dawa za kulevya

BIASHARA haramu ya madawa ya kulevya imedaiwa kushamiri katika mtaa wa Sinani Manispaa ya Mtwara-Mikindani na hivyo kuathiri afya za watumiaji na usalama wa eneo hilo.

Uchunguzi uliofanywa na KUSINI hivi karibuni umebaini kuwa ‘unga’ huuzwa bila mficho kwa muhitaji huku mamlaka husika zikikaa kimya.

Kufuatia hali hiyo Diwani wa kata ya Vigaeni Saidi Ali Nassor (White) amesema atasimamia mchakato wa upigaji kura za siri kwa wakazi wa mtaa wa Sinani katani humo kubaini watu wanaojihusisha uuzaji wa madawa hayo ya kulevya

Akizungumza katika mkutano wa adhara kwa wakazi wa mtaa huo jana, White alisema katika manispaa hiyo biashara ya madawa ya kulevya hufanyika katika mtaa huo hali ambayo licha ya kuadhiri vijana pia inatishia usalama wa wakazi wake.

Alikiri biashara haramu ipo dhahiri katika maeneo mbalimbali ya mtaa huo na kwamba ili kukabiliana na hali hiyo anatarajia kuendehsa kura za maoni kwa wakazi wa maeneo hayo ili watakaobainika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Wanaouza madawa tunawafahamu, tunaishi nao…sasa nasema hivi nitandaa utaratibu wa kupiga kura za siri kuwabaini wauza madawa hayo…yule atakayetajwa mara nyingi bila shaka atakuwa anahusika…licha ya kuathiri vijana wetu lakini pia hutuondolea amani katika eneo letu, mtaa wa Sinani si amani tena” alisema diwani huyo

Dawa za kulevya aina ya Heroine

Aliongeza kuwa “Kwa kushirikiana na polisi kata tutahakikisha wale wote watakaobainika tunawachukulia hatua za kisheria…haya madawa yanauzwa nje nje hayana mficho, kama mnavyojua watumiaji wa madawa haya wanageuka kuwa vibaka, wezi, jambo ambalo ni hatari kwa usalama”

Hata hivyo diwani huyo hakueleza lini kura hizo zitapigwa licha ya kuahidi kuwa haitachukua mda mrefu kutekeleza adhima hiyo ili kurejesha hali ya utulivu katika eneo hilo.

Diwani huyo alilazimika kutangaza hatua hiyo baada ya wananchi wa mtaa huo kumlalamikia kuwa wamekuwa wakiishi kwa hofu kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uporaji vinavyoendeshwa na vijana wanaotumia madawa ya kulevya yanayouzwa katika maeneo hayo.

Zaituni Zawadi mkazi wa mtaa huo alimweleza diwani huyo kuwa mtaa wa Sinani ambao ndiyo kielelezo cha Manispaa ya Mtwara-Mikindani hauna amani kutokana na vijana wanaotumia madawa ya kulevya kuendesha vitendo vya uporaji wa mali na kudhuru raia wema.

“Siku hizi tunalazimika kujisaidia ndani kwa hofu ya kuvamiwa iwapo utatoka nje kujisaidia…maisha yetu yamekuwa si ya mani tena, wanaosababisha hayo tunawajua…wanauza unga kwa vijana wetu… tunaomba msaada wako mheshimiwa diwani” alisema Zawadi huku akishangiliwa na wakazi waliohudhuria mkutano huo.

Mkazi mwingine Amina Dogoa alisisitiza kuwa hali si swari katika mtaa huo na kwamba hali hiyo inasababishwa na eneo hilo kugeuzwa kuwa soko la madawa ya kulevya.

“Mimi mwenyewe juzi nilinusurika kuporwa, kama si jitihada zangu ningeporwa, kwa kweli hali si swari…wanaofanya haya ni vijana wetu wanaotumia unga, na hawa vijana wanaathiri sana eneo letu kwa sababu ndiko madawa hayo ynapatikana” alisema Dogoa

Mwisho

Advertisements