DIWANI ADAIWA KUBADILISHA NJIA KUKWEPA WAPIGA KURA

WAKAZI wa kijiji cha Mayaya kata ya Tangazo wilaya ya Mtwara mkoani hapa, wamemkataa diwani wao mbele ya mkuu wa wilaya hiyo wakidai amebadilisha njia kukwepa kuonanan na wanakijiji hao.

Wanakijiji hao walimweleza mkuu wa wilaya hiyo Wilman Ndile aliyekwenda kijijini hapo kujitambulisha akiwa ameongozana na diwani huyo mwishoni mwa wiki , kuwa hawamtaki diwani wao, Mohamedi Saidi (Nakatamtende) kwa madai tangu achaguliwe mwaka 2010 hajawahi kukanyaga ardhi ya kijiji hicho.

Walisema kuwa kwakuwa mkuu wa wilaya amekuja na diwani huyo basi ahakikishe anaondoka naye mara baada ya kumaliza mkutano huo  na kwamba hata kuwapo kwao mkutanoni hapo ni kwasababu yeye mkuu wa wilaya aliwaalifu mkutano huo ni wake.

Sokomoko hilo lilianza baada ya mkuu wa wilaya kuhutubia akifuatiwa na wataalamu wengine kutoka halmashauri ya wilaya na kisha kuwataka wakazi wa kijiji hicho kutoa kero zao ili aone namna ya kuzipatia majibu ndipo kila mkazi aliyesimama alidai kero yake ni kuwapo kwa diwani huyo mkutanoni hapo huku akijua kuwa tangu walipomchagua hajawahi kuwatembelea.

“Wewe (DC) umeripoti kazini mwezi mmoja tu uliopita leo umefika kijijini kwetu sasa huyo miaka miwili nini kinamkwaza asije kujua matatizo yetu?… lakini hata kukatisha hapa hajawahi na njia kabadilisha akitoka kijijini kwake hapo Tangazo hapiti hapa anazunguka huko…tena umuondoe huko mbele hatumtaki hata kumuona”, alisema Masoud Nalyogo huku umati wa wakazi wenzake wakishangilia na kuzomea.

Wimbi hilo la kukataliwa diwani Nakatamtende, halikuishia hapo kwani kila aliyesisimama alirusha ‘makombora mazito’ kwa diwani huyo ambaye wakati wote alijiinamia pembeni ya mkuu wa wilaya.

“Mkuu wa wilaya tumekusikia, hapa kila ulipoongea ulisema diwani wenu, diwani wenu…tena ulisisitiza eti yeye ndiye kakuambia kero zetu sasa ebu wewe muulize alikuja hapa lini na sisi tukamwambia hizo kero…sisi ndio tunamuona hapa tangu tulipomchagua miaka miwili iliyopita” alisema Hassan Maoud mkazi wa Mayaya.

Baada ya madai hayo ya wananchi ndipo mkuu wa wilaya aliposimama ili kujibu baadhi ya kero zilizoibuliwa na wakazi hao na alipofika suala la diwani alisema hawezi kujibia kwa kuwa muhusika yupo mkutanoni hivyo anawajibika kujibu hoja zake.

Diwani Nakatamtende aliposimama ili kuongea na wananchi alizomewa na huku wengine wakiinuka kuondoka mkutanoni hali iliyowafanya maafisa walioongozana na mkuu huyo wa wilaya kuwarai wasiondoke wamsikilize ni kwanini hajawahi kufika kijijini hapo umbali wa kilometa zisizozidi kumi kutoka makao makuu ya kata ambako ndio anakoishi diwani huyo.

Wakazi hao walirejea kumsikiliza diwani wao ambaye alijieleza kuwa ameshindwa kufika kijijini hapo kwakuwa ana maeneo saba ya kutembelea na amejiwekea utaratibu wa kutembelea kila eneo baada ya miezi mitatu hivyo hadi anafika eneo la mwisho ni miaka miwili.

“Jamani mimi bado nawapenda nitakuja tu maana licha ya kuwa na vijiji vitano katika kata yetu hii lakini nina maeneo saba ya kuyatembelea na kila eneo natembelea baada ya miezi mitatu sasa mtaona nilivyo bize”, alisema diwani huyo na kuibua zogo mkutanoni hapo huku wananchi wakimwambia ni mwongo.

Kuona hivyo mkuu wa wilaya alimrudisha diwani kitini ili mwenyekiti wa kijiji afunge mkutano maana watu wengi walikuwa wameshaondoka kukwepa kumsikiliza diwani huyo, na ndipo mkutano ulipofungwa na diwani alipewa ulinzi na askari polisi baada ya kuzongwa na wananchi.

Mwisho.