VIJIJI VINAVYOCHIMBWA GESI MTWARA HAVIJANUFAIKA NA RASILIMALI HIYO

TAARIFA ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) kwa halmashauri ya wilaya ya Mtwara mkoani hapa imebainisha kuwa wakazi wa maeneo yanayochimbwa gesi wilayani humo hawajanufaika na rasilimali hiyo licha ya kuanza kutumika.

Akiwasilisha taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa serikali ya mwaka 2010/11 katika kikao cha baraza la madiwani wa halmshauri hiyo kilichoketi jana mjini Mtwara, mkaguzi mkazi mkoani Mtwara, Hassan Kaku alisema wanavijiji wanaozunguka maeneo ambayo gesi hiyo inachimbwa hawajanufaika na rasiliamali hiyo licha ya kuanza kuwanufaisha watu wengine kwa kuzalisha umeme.

“Bado vijiji vinavyozunguka eneo ambalo gesi asilia inachimbwa havijanufaika na rasilimali yao…vijiji hivyo havina umeme, licha ya kwamba gesi inayozalishwa hutumika kuzalisha umeme unaotumiwa na watu wengine…hili ni eneo linalohitaji kufanyiwa marekebisho” ilibainisha sehemu ya taarifa hiyo

“Ushauri wetu kwa halmashauri ya wilaya ni kupitia upya mkataba huo ili kuhakikisha vijiji hivyo vinanufaika na rasilimali yao” ilishauri taarifa hiyo.

Kaku alieleza kuwa licha ya halmashauri hiyo kupata hati inayorizisha yenye mambo ya kutilia mkazo, bado taarifa hiyo imedokeza kuwa ni muhimu kwa halmashauri hiyo kuhakikisha vijiji hivyo vinanufaika na gesi ili thamani ya rasilimali hiyo iweze kuonekana kwa jamii hiyo.

Kufuatia taarifa hiyo baadhi ya madiwani walionesha kuguswa na kuchangia kwa kuitaka halmshauri kutoingia mikataba kama hivyo kabla ya kuthibitishwa na kikao cha baraza la madiwani.

“Hatuwatendei haki, wakati sisi tunafurahia umeme wa uhakika, wanakijiji ambao wameitunza rasilimali hii kwa miaka mingi wapo gizani …waliambiwa wafanye ‘wiring’ (kutandaza nyaya kwenye nyumba) wamefanya hivyo, waliambiwa walipie gharama kidogo wamefanya hivyo lakini bado hawajapata umeme” alisema Hassan Mauji diwani wa kata ya Nanyamba

Aliongeza kuwa “Nyumba za jamii, shule, misikiti waliambiwa wafanye wiring halafu wataunganishiwa umeme bure, wamefanya hivyo lakini hadi leo hawajunganishiwa umeme …pale kwetu Nanyamba watu 60 wapo tayari kuunganishiwa umeme hadi leo hatujapata, cha ajabu kuna minara mitatu ya simu wao wameunganishiwa..naomba watendaji wasisaini mikataba kama hii kabla ya baraka za baraza”

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Wilman Ndile ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Mtwara alisema ameguswa na taarifa hiyo na kuahidi kuwasiliana na shirika la umeme Tanesco kubaini tatizo la kutounganishiwa umeme kwa wakazi wa vijiji hivyo ambapo pia waliwaomba madiwani kutojadili kwa kina kipengere hicho kwa kuwa kikao hicho si maalum kwa suala hilo.

“Ni suala nyeti, nitaongea na Tanesco kuona tatizo nini…mkaguzi ametukumbusha kuwa wananchi wana haki ya kunufaika na rasilimali zao na ni jukumu letu kuhakikisha hilo…lakini niwakumbushe kuwa hiki si kikao halali cha kujadili suala hilo kwa kina naomba tuliingize katika vikao vyetu vingine” alisema Ndile

Naye mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Saidi Ndazigula alisema ni wakati muafaka kwa wana-Mtwara kuhakikisha wanafaidika na rasilimali zao kabla ya maeneo mengine.

“Ukimuona mtu ana wasiwasi basi ujue huyo mtu ana akili, anafahamu nini kinaweza kutokea…tupo kwenye wasiwasi…tunahisi wapo watakaochukua rasilimali yetu na sisi kutuacha patupu…ni muhimu kulijadili hili katika vikao vyetu vijavyo.

Mwisho