102 MILIONI ZAYENYUKA MTWARA

MILIONI 102.6 za Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) hazijulikani zilipo baada ya Hazina kudai wamezituma kwa halmshauri ya wilaya ya Mtwara ambayo imesema haijazipokea fedha hizo hadi sasa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2010/11 kwa halmshauri hiyo, fedha hizo zilitumwa katika kipindi cha mwaka huo wa fedha wa serikali.

Akiwasilisha taarifa hiyo katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichoketi juzi mjini Mtwara, Mkaguzi Mkazi wa mkoa wa Mtwara, Hassan Kaku alisema ‘kitendawili’ hicho kimeitia doa halmshauri hiyo, pamoja na mambo mengine kimesababisha kupata hati inayorizisha yenye mambo mawili ya kulitia mkazo likiwapo la fedha hizo.

“Kumbukumbu kutoka hazina zinaonesha kuwa ilituma 102,609,000 kwa halmshauri ya Mtwara lakini halmashauri imekana kuzipokea fedha hizo hadi leo” alisema Kaku akiwasilisha taarifa hiyo.

Aidha katika hatua nyingine mkaguzi huyo alisema halmashauri hiyo ilishindwa kuendana na sheria ya mfuko wa pensheni ya watumishi wa serikali za mitaa (LAPF) ambapo halmashauri haikuchangia makato ya watumishi kwenye mfuko huo na kusababisha kutozwa riba ya sh. 82,719.000.

Baada ya kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Idd Mushiri alisimama kutoa ufafanuzi kwa kueleza kuwa jitihada mbalimbali zinafanywa na halmshauri yake kuwasilina na hazina ili kujua mahala ambapo fedha hizo zimekwama na kisha kuzituma tena kwa halmashaurihiyo.

“Suala hili tumelifanyia kazi kwa mda mrefu sasa tangu hoja hiyo iwasilishwe na wakaguzi, hadi sasa fedha hizo hatujazipata na tunaendelea na mzungumzo ya Hazina ili hatimaye tuzipate na tutekeleze miradi kusudiwa…hizi ni fedha za MMES” alisema Mushiri

Akizungumzia 82.7 za LAPF, mkurugenzi huyo alieleza kuwa tatizo hilo lilijitokeza kutokana na mfuko huo kusuasua kiutendaji hali iliyosababisha fedha za watumishi hao kukatwa na serikali za mitaa.

“Serikali za mitaa ilikuwa inakata hizi fedha wakati mfuko wenyewe ukiwa hoi kiutendaji, ulipokuja kuinukia walikuja na madi kuwa hatujawalipia watendaji wetu michango katika ofisi yao…walikuwa wanaangalia mtumishi alipoajiriwa na kuana kufanya mahesabu, tulijaribu kuwaeleza hali halisi lakini hakuna aliyetuelewa” alifafanua mkurugenzi huyo.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Wilman Ndile alipongeza halmshauri hiyo kwa kupata hati safi na kuwataka madiwani kuzidi kusimamia matumizi sahihi ili kumaliza hoja za wakaguzi zinazotia doa hati hiyo.

“Hapa ni sawa mtu amevaa shati jeupe nzuri lakini lina doa jeusi…hizi kasoro hazina budi kumalizwa, na hiyo inawezekana…mkifanya vizuri katika hilo, madiwani mutaonkeana munafanya kazi vizuri, mani pia nitaonekana nafanya kazi vizuri na hatimaye serikali kwa ujumla itaonekana nzuri” alisema Ndile

Mwenyekiti wa halmshauri hiyo Saidi Ndazigula alisema kwisha kwa mahesabu hayo ni mwanzo wa ukaguzi wa hesabu zinginehivyo ni jukumu la kila mtendaji kuhakikisha anamaliza kasoro katika matumizi ya fedha hizo.

mwisho