Korosho hatarini kufa Mtwara, tani 300 za viwatilifu ‘feki’ zanaswa

Mkaguzi Mkuu wa Afya ya Mimea Nchini, Cornelius Mkondo alionesha viwatilifu aina ya salfa ya vumbi alivyokamata katika ghala la Export Trading Company Ltd, mjini Mtwara

ZAO kuu la biashara kwa wakazi wa mkoa wa Mtwara la Korosho limo hatarini kuporomoka uzalishaji wake kutokana na kuingia kwa viwatilifu bandia na kusambazwa kwa wakulima wa zao hilo.

Hali hiyo imebinika jana baada ya Serikali kukamata tani 300 za viwatilifu aina ya sulfa ya vumbi ambayo haioneshi mwaka iliyotengenezwa wala tarehe ya mwisho wa kutumika katika ghala la kampuni ya Export Trading Company Ltd, lililopo mjini Mtwara.

Kukamatwa kwa kiasi hicho kikubwa cha viwatilifu hivyo kunatokana na ukaguzi wa kushtukiza uliofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Afya ya Mimema nchini, Cornelius Fabian Mkondo kwa maghala yanayohifadhi viwatilifu hivyo mjini Mtwara.

Viwatilifu hivyo vyenye jina la biashara Falcon-S Dust licha ya kukosa mahali panapoonesha muda wa kutengenezwa na mwisho wa kutumika, pia vimekutwa vikiwa vimeganda mithili ya jiwe ili hali ni kiwatilifu cha vumbi.

Mkondo alisema kuwa kumbukumbu zilizopo katika mifuko iliyotumika kuhifadhia dawa hizo zineonesha kuwa zimetengenezwa nchini India na zipo kwa majaribio hivyo haziruhusiwi kusambazwa kwa wakulima.

“Hapa zinaonesha zipo kwa majaribio, hivyo ni kosa la kisheria kuwasambazia wakulima…zinatakiwa zifanyiwe majaribio kwa misimu mitatu halafu mamlaka husika ithibitishe…haina mwaka uliotengenezwa wala mwisho wa kutumika kwake…yenyewe pia badala ya kuwa vumbi, imeganda” alisema Mkondo

Alifafanua kuwa “Naizuia dawa hii kwa sasa isisambazwe kwa wakulima, nitachukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi na kama itabainika haifai kwa matumzi, itatekezwa na gharama hizo zitakuwa za kampuni hii …kwa kweli tukienda na mwendo huu zao la korosho litakufa hapa Mtwara”

Hali hiyo imejitokeza wakati madiwani wa halmshauri ya wilaya ya Masasi, mkoani hapa katika kikao cha baraza lao kilichoketi hivi karibuni wakilalamikia kusambaziwa viwafitifu aina ya salfa ya vumbi, iliyoganda na hivyo kuwalazimu wakulima kuitwanga kwenye vinu ili wapate unga.

Mmoja wa madiwani hao, Victor Mmavele alikiambia kikao hicho kuwa wakulima katika kata yake ya Nanjota ni miongoni mwa waliokutana na adha hiyo na kuhoji zilipo mamlaka husika wakati wakulima hao wakidhulumiwa kwa kuuziwa dawa bandia.

“Kule kwetu tumeletewa salfa iliyoganda, tunaitwanga kwenye vinu ili tupate unga wa kupuliza kwenye mikorosho yetu…ile salfa ni ngumu kiasi inapasua vinu vetu…hivi teknolojia hii imeanza lini? Mamlaka huska zipo wapi?” alihoji Mmavele

Hali ya usambazaji wa pembejeo za ruzuku mkoani humo imeendelea kuwa tete hali inayosababisha wakulima washindwe kuihudumia mikorosho yao na hivyo kuwapo na uwezekano mkubwa wa kushuka kwa kiwango cha uzalishaji.

Boharia wa kampuni hiyo ambayo ni miongoni mwa makampuni yaliyopewa zabuni ya kusambaza viwatilifu vya ruzuku vya korosho kwa walima, Dismas Mtuhi alikiri kukutwa kwa tani hizo 300 za salfa ya vumbi zikiwa zimeganda katika ghala lake na kuongeza kuwa zililetwa katika ghala hilo kwa makosa na kwamba lengo lilikuwa  kuzipeleka katika machimbo ya madini.

“Tumezipokea tangu Machi, mwaka huu, baada ya kuziona zimeganda tulizizuia, hatukusambaza kwa wakulima…hizi zililetwa huku kwa makosa, zilikuwa zinaenda machimbo ya madini…zipo tani 300” alisema Mtuhi

Aidha katika ghala la Kampuni ya Mocrops Tanzania, mkaguzi huyo alibaini kuhifadhiwa kwa viwatilifu katika ghala ambalo halipitishi mwanga wa kutosha na hivyo kuwepo kwa uwezekano wa kuathiri ubora wa dawa hizo.

“Mocrops Tanzania tumebaini na kushauri lile ghala waweke maeneo ya kupitishia mwanga, kwa hali ilivyo dawa zikiwa nyingi zinaweza kulipuka…pia ubora unaweza kushuka” alisema mkurugenzi huyo

Mwisho

Advertisements