TCCIA YAPINGA GESI YA MTWARA KWENDA DAR

CHAMA cha Wafanyabishara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) mkoani Mtwara kimepinga vikali uwamzi wa Serikali wa kujenga bomba litakalosafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam kwa madai uwamuzi huo utawakimbiza wawekezaji mkoani humo na kusababisha uendelee kuwa masikini.

Akisoma tamko la chama katika mkutano wake mkuu uliofanyika jana mjini Mtwara, Makamu Mwenyekiti Biashara, Alhaji Shaibu Namkuna alisema serikali haikuwashirikisha wananchi katika kufikia uwamzi huo ambao aliuita wa kibabe.

Alifafanua kuwa kitendo cha kusafirisha gesi kitawafukuza wawekezaji Mtwara kwa madai hawatakuwa na sababu ya kuwekeza katika mkoa huo ili hali gesi ambayo ingekuwa kivutio kikubwa kwao inapatikana jijini Dar es Salaam.

“Sisi kama TCCIA tumeuona uwamuzi huo si wa haki kwa wananchi wa mkoa wa Mtwara, kwanza kabisa haukuwa shirikishi, pili utapunguza kasi na uwingi wa wawekezaji mkoani Mtwara, wawekezaji hawataona umuhimu wa kuwekeza Mtwara wakati anaona kuna uhakika wa kupata nishati hiyo akiwa Dar es Salaam na hivyo kuchangia mrundikano wa viwanda katika jiji lile” alisema Namkuna

Aliongeza kuwa “Kusafirishwa kwa gesi hiyo pia kutaathiri upatikanaji wa ajira kwa vijan wa mkoa wa Mtwara ambao wameshiriki toka mwanzo katika shughuli zote za utafiti kama vibarua, aidha vijiji vya Mtwara vitaendelea kukosa maendeleo na kubaki masikini uliokithiri”

Alibainisha kuwa TCCIA mkoa wa Mtwara inaungana na wananchi wote wa mkoa wa Mtwara wanaonesha wasiwasi juu ya uwamzi huo wa serikali na kutamka rasmi kuupiga.

“Tunapenda kutamka kwamba tunaupinga uwamuzi huo, badala yake tunashauri mazao ya gesi ndiyo yasafirishwe…wajenge mitambo ya kufua umeme halafu umeme utakaozalishwa ndiyo uunganishwe kwenye gridi ya Taifa, makao makuu yake yawe Mtwara” alisisitiza makamu mwenyekiti huyo

Aliongeza kuwa “Kwamba umeme utokanao na gesi hiyo utosheleze mahitaji ya Mtwara, kwa kuufikisha vijijini ili kuinua viwanda vidogovidogo vya ubanguaji wa korosho, usindikaji wa matunda na mbegu za mafuta na muhogo ili kupanua ajira na kuongeza thamani ya mazao hayo.

Taarifa hiyo iliendela kuishauri serikali kuweka wazi mikataba inayoingia na wawekezaji ili wananchi wa mkoa wa Mtwara wajuwe watafaidikaje na shuguli hizo kama ilivyo maeneo mengine uku akitolea mfano maeneo ya machimbo ya dhahabu, almasi na madini mengine.

“Viongozi wetu hawana upeo wa kutosha, japokuwa wamesoma lakini hawajui wanachokifanya, wana macho hawaoni, wana masikio hawasikii na sisi tuwe mambumbumbu kama wao? Nasema hili haliwezekani, wana Mtwara wapo kwao na mwenye kwao yeyote anatetea ngao ya kwao” alisema Polle Polle mmoja wa wajumbe wa mkutano huo akichangia tamko hilo.

Mwenyekiti wa chama hicho, Saidi Nahunda alisema serikali inapaswa kuangalia upya uwamuzi wake wa kupeleka gesi asilia dare s Salaam kwa kuwa maamuzi hayo hayakushirikia wananchi wa eneo huska.

Mwisho

 

 

 

Advertisements