RC Mtwara akerwa Manispaa kupora ardhi za wanyonge

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia

MKUU wa Mkoa wa Mtwara Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia amesema alichukua uwamuzi wa kusitisha upimaji na ugawaji wa viwanja katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani baada ya kukerwa na ‘uporaji’ wa ardhi ya wanyonje kwa visingizio vya kukua kwa kasi ya ujenzi wa manispaa hiyo.

Simbakalia alilazimika kuvunja ukimya huo mwishoni mwa wiki baada ya madiwani wa manispaa hiyo kumrushia ‘madogo’ wakilaani kitendo cha kusitisha zoezi hilo kwa madai linakaribisha ujenzi holela na kuzua malalamiko kwa wananchi wanaohitaji viwanja kwa ajili ya makazi.

“Mkuu wa mkoa aliyesitisha zoezi la upimaji na ugawaji wa viwanja yupo hapa na anasikia malalamiko haya ya wananchi kupitia madiwani sisi…kasi ya ujenzi holela inaongezeka na sisi madiwani tunalaumiwa na wananchi” alisema Rukia Mikidadi diwani viti maalum katika kikao cha baraza la madiwani.

Kauli hizo na nyingine zilizotolewa na madiwani hao, zilimfanya mkuu huyo wa mkoa kutoa kile alichokiita ufafazi wa sitisho lake kuwa wakazi wa asili katika maeneo hayo walikuwa wananyang’anywa ardhi yao na kupewa watu wengine, kitendo ambacho alisema si haki.

“Nimepokea malamiko mengi kutoka kwa wananchi…kule Mitengo kali zaidi ni pale wananchi wanaponyang’anywa  ardhi yao na kupewa watu wengine kwa kisingizio cha kasi ya ukuaji wa mji…hili halikubaliki nipo hapa kusimamia haki” alisema Simbakalia

“Wanaodhulum ardhi ya wanyonge wapo humu ndani wapo, nawafahamu…tukienda kule na kuhakiki kiwanja kimoja badala ya kingine hatutatazamana usoni…jamani tunakwenda wapi?” alihoji huku akionesha kukerwa na jambo hilo

Simbakalia alifafanua kuwa katika maeneo ambayo wananchi walikuwa wanatumia kama mashamba, waliondolewa na manispaa hiyo kwa kulipwa fidia ya sh. 100 kwa mita moja ya mraba na kisha kutakiwa kununua ukubwa wa eneo hilo hilo kwa sh. 1200.

“Wewe umemlipa fidia ya sh. 100 kwa mita moja ya mraba halafu unamuuzia sh. 1200, hivi kuna haki hapo? Na unamwambia kama huna ondoka …hili ni eneo lake la asili kwa nini anyang’anywe kwa kigezo cha kasi ya kukua kwa mji…nasema haiwezekani” alisisitiza Simbakalia na kuongeza

“Huu ni mji wa watu wa Mtwara si mji wa wawekezaji…hakuna kasi ya ujenzi wowote kule kwenye vile viwanja, kasi iliyopo ni ya kugawana viwanja na kupora ardhi ya wakazi wa Mtwara…kwa nini msimgawie kiwanja kisha mukamwambia alipie sh. 20,000 au 30,000 lile eneo lake”

Alisisitiza kuwa katika kutetea haki ya wanyonge katika ardhi yao hana mzaha nalo na yupo tayari kushtakiwa kwa mamlaka yeyote ya juu yake na si kuona wenyeji wakinyang’anywa ardhi yao na wajanja wachache.

Mstahiki Meya wa manispaa hiyo, Suleiman Mtalika (shilingi) alikiri manispaa yake kugawa viwanja kwa gharama kubwa inayowanyima haki wanyonge kumiliki ardhi huku wamiliki wa asili wa maeneo hayo wakijikuta wanaporwa ardhi yao.

“Ni kweli gharama hizi kwa wananchi wa kawaida ni kubwa…nakuahidi mkuu wa mkoa tutalifanyia kazi” alisema Shilingi

Mwisho

 

Advertisements