Stakabadhi Ghalani hatarini kufa Mtwara

Korosho ghalani

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Joseph Simbakali

VYAMA vya Msingi vya Ushirika wa Kilimo na Masoko vya wilaya ya Mtwara, Masasi na Nanyumbu mkoani Mtwara vimetishia kujiondoa katika mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani unaotumika katika ununuzi wa zao la Korosho kwa madai umekuwa tishio kwa mali na usalama wao.

Wakizungumza katika mkutano mkuu wa 13 wa chama kikuu cha ushirika cha wilaya hizo (Mamcu) uliofanyika mwishoni mwa wiki mjini Masasi, viongozi wa vyama hivyo walisema hawapo tayari kuendelea na mfumo huo iwapo viongozi wa kisiasa na serikali wataendelea kuingilia utendaji kazi wao.

Walisema msimu uliopita wa ununuzi wa zao hilo, ulitawaliwa na maagizo ya viongozi wa serikali na kuweka kando kanuni na sheria za mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani hali iliyosababisha kuyumba kwa soko la zao hilo na kuvisababishia vyama na wakulima kupata faida ndogo.

“Biashara ilitawaliwa na siasa…mbaya zaidi mkuu wa mkoa (Joseph Simbakalia) sijui kwa makusudi au kwa kutofahamu akaagiza tulipe malipo ya tatu wakati vyama havina fedha kabisa…watu tumefungiwa katika maghala, tumetishiwa kuuawa, tumemwagiwa maji ya upupu na wakulima wanaodai malipo ya tatu ilihali chama hakina fedha” alisema Edward Mahelela katibu wa chama cha msingi Chikolopola

Aliongeza kuwa “Wakulima wanasema mkuu wa mkoa kaagiza tuwalipe, na ni kweli mkuu wa mkoa ameagiza hivyo…watu wamevunjiwa nyumba zao, zingine zimechomwa moto…hadi leo wapo viongozi wa ushirika wanaoishi uhamishoni kwa kuhofia usalama wao…hakuna wa kututetea wala kutulinda”

Alifafanua kuwa kutokana na hali hiyo vyama hivyo vinaona bora vijiondoe kwenye mfumo huo wa ununuzi wa mazao ili waendeshe ushirika kama ilivyokuwa awali kabla ya mfumo kwa lengo la kunusuru mali na maisha yao.

Chini ya mfumo wa Stakabadhi ya Mazao Ghalani vyama vya msingi vya ushirika wa kilimo na masoko vinakusanya korosho za wakulima na kuzipeleka kwenye mnada baada ya kuwalipa malipo ya kwanza ambayo yanatokana na vyama hivyo kukopa benki asilimia 70 ya bei dira na kwamba iwapo tishio hilo litatekelezwa mfumo huo utakuwa umefikia mwisho.

korosho

“Kama serikali inataka tuendelee na mfumo huu basi tukubaliane kuwa asilimia 70 ya faida ya biashara alipwe mkulima na asilimia 30 ibakie kwenye vyama ili kuimarisha vyama husika…ushuru wa sh. 50 kwa kilo tunaopata unaishia kugharamia safari za viongozi wa vyama kupeleka mzigo ghalani…msimu ukiisha chama hakina kitu “ alibainisha Mahelela

Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Mrina, Rashidi Mtingala alidai kuwa vyama vyote 87 vya wilaya hizo vipo tayari kujiondoa kwenye mfumo huo, pia iwapo viongozi wa serikali wataendelea kutoa amri zinazoathiri mwenendo wa soko la korosho wakati wa minada na maagizo yasiyozingatia hali ya biashara.

“Tunahitaji biashara huru, wacha biashara ijiendeshe yenyewe, tusichanganye siasa na biashara…serikali isiwaone bora wakulima ikavisahau vyama vya msingi ambavyo ndiyo walezi wa wakulima…leo sisi tunaonekana wezi kila tunapopita…hili hatulikubali ni heri tujiondoe katika mfumo huu” alisema Mtingala huku akiungwa mkono na wajumbe wa mkutano huo.

Viongozi hao chini ya mwenyekiti wa Mamcu, Fikiri Makalani walikubalina kuunda kamati ya watu wachache kwenda kuongea na mkuu wa mkoa ili kumfikishia adhima yao ya kujitoa katika mfumo huo iwapo madai yao hayatasikilizwa.

“Wajumbe wa kamati nitawateua kutoka miongoni mwenu haraka iwezekanavyo ili tukaonane na mkuu wa mkoa na kumweleza adhima hii ya kujiondoa kwenye mfumo iwapo madai yenu yatapuuzwa” alisema Makalani

Kwa upande wake mgeni rasmi katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmshauri ya Wilaya ya Nanyumbu, William Dua alisema madai hayo ya viongozi wa ushirika ni ya msingi licha ya kuwataka kuwa na subira.

“Madai yenu ya msingi kabisa, nimeyasikia na nitayafikisha…kuweni na subira wakati tunaandaa utaratibu wa kukifikisha kilio chenu kwa viongozi huska” alisema Dua

Mwisho

 

 

 

 

Advertisements