Matonya afariki dunia

Mzee Paulo Mawezi maarufu kama Matonya akiwa na mwanae Elizabath katika Kijiiji cha Mpamantwa Tarafa ya Bahi Mkoani Dodoma. Picha hii ilipigwa 2010 wakati alipokwenda kwa mapumziko ya sikukuu ya Krismas

LICHA ya umaarufu mkubwa aliokuwa nao na kufahamika katika miji mingi nchini, ombaomba Paul Mawezi maarufu kwa jina la Mzee Matonya, amefariki dunia na kuzikwa katika mazingira ya ufukara mkubwa.

Matonya alizikwa jana kijijini kwake Mpamantwa, Wilaya ya Bahi, Dodoma akiwa amevishwa nguo moja nyeusi, huku mwili wake ukibebwa na watu wasiozidi 20, waliotumia ngozi kuu kuu ya ng’ombe.

Matonya aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kikohozi tangu Mei mwaka huu, alifariki dunia juzi usiku na kuzikwa jana saa saba mchana mita tatu kutoka katika nyumba yake ya tembe alimokuwa akiishi.

Ndugu na jamaa zake wa karibu walisema Matonya ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 90, hakuwahi kwenda kutibiwa hospitali kutokana na ukosefu wa fedha.

Mwandishi wetu alishuhudia idadi ndogo ya waombolezaji nyumbani kwa Matonya, huku watoto wake watatu waliokuwapo msibani hapo kati ya watano aliowaacha hai, wakisema kuwa baba yao amefariki kutokana na umaskini na ufukara.

“Hatukuweza kumpeleka hata hospitali kupata vipimo kwani hatukuwa na uwezo wa kwenda mjini Dodoma kutokana na kukosa hata nauli, ndiyo maana tumekuwa kimya hadi Mungu alipomchukua,’’ alisema mmoja wa watoto hao, David Paulo.

Source http://www.mwananchi.co.tz

 

Advertisements