Polisi wachukua bastola ya Ligwangala

SAKATA la  makada wa CCM, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangala kutoleana bastola, limechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumnyang’anya bastola Kigwangala huku likianza  kuwahoji wapambe wa mahasimu hao.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, (RPC) Antony Lutta zilieleza kuwa jeshi hilo linaishikilia silaha ya Dk Kigwangala hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

Kauli hiyo ya polisi imekuja siku moja baada ya  uongozi wa chama hicho Wilaya ya Nzega, kutaka suala hilo liondolewe polisi ili walishughulikie kimyakimya ndani ya chama.

Mwananchi Jumapili lilipomtafuta Dk Kigwangala ambaye pia ni Mbunge wa Nzega na kumuuliza kuhusu suala hilo alisema: “Bastola yangu mbona ninayo, hilo halina ukweli, bastola ninayo hapa.”

Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa CCM wilayani humo umempa onyo kali Dk Kigwangala ukieleza kwamba endapo ataendeleza msimamo wake wa kukataa kuhojiwa na chama, atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa kadi ya uanachama.

Kujiuzulu ubunge
Hata hivyo, mbunge huyo alisema kuwa hana imani na uongozi wa CCM wilayani Nzega na kwamba iwapo CCM mkoa na taifa hautaingilia kati mgogoro huo, yuko tayari kujiuzulu ubunge.
 
Bashe na Dk Kigwangala ambao ni  mahasimu wa siku nyingi katika medani za siasa wilayani Nzega walidaiwa kutoleana bastola Alhamisi iliyopita walipogongana katika ofisi za CCM wilayani humo, wakati  wakirejesha fomu za kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia wilaya hiyo.

Hata hivyo, pamoja na taarifa hizo kuthibitishwa na viongozi wa CCM wilayani humo na RPC Lutta, kila mmoja alikanusha madai hayo akimtuhumu mwingine kuwa ndiyo chanzo cha ugomvi huo.

Wakati Bashe alisema Dk  Kigwangala ndiye aliyetoa bastola kumtishia wakiwa ndani ya Ofisi ya CCM Wilaya, Dk Kigwangala alieleza kuwa walinzi wa Bashe ndio waliomtishia yeye bastola na kwamba tayari amelifikisha suala hilo polisi na wanalifanyia kazi.
 
Kauli ya Kamanda Lutta
Jana Lutta alisema ingawa imemnyang’anya bastola Dk Kigwangala, mbunge huyo anamiliki silaha hiyo kihalali.

“Taarifa zao tutazitoa baadaye  kwa sababu hivi sasa tunakusanya ushahidi na tunawahoji wapambe wao, ambao inasemekana wakati tukio linatokea walikuwepo eneo hilo,” alisema Lutta na kuongeza:

“Silaha yake ipo katika Kituo cha Polisi Nzega, uchunguzi tulioufanya unaonyesha kuwa ni yake, anaimiliki kihalali. Ni kweli ndugu yangu silaha yake tunaishikilia.”

Alisema kuwa kazi  ya polisi ni kuchunguza tukio zima na ikikamilisha uchunguzi wake, itaupeleka katika mamkala husika.

Source www.mwananchi.co.tz

Advertisements