WAKULIMA WATAKA KIINUA MGONGO, FIDIA

Mkulima wa Nanyumbu, Thabiti Geugeu

WAKULIMA wa wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, wametaka katiba ijayo itamke wazi kuwalipa kiinua mgongo na fidia wakati mavuno yanapokosekana kwa sababu za kimazingira na mabadiliko ya tabianchi.

Wakulima wamesema hayo juzi walipokuwa wakichangia mada katika mdahalo uliofanyika katika kijiji cha Mangaka wa kuwajengea uwezo kuchangia juu ya mabadiliko ya katiba mara tume hiyoa itakapofika wilayani humo.

Katika mdahalo huo ulioitishwa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani Mtwara (Mrengo) na kufadhiliwa na The Foundation for Civil Society, liojumisha maakundi mbalimbali ya jamii wakiwemo wakulima, wajasiliamali na walemavu, wakulima hao walisema katiba ya sasa licha ya kutamka wazi kuwa nchi hii ni ya wakulima na wafanyakazi lakini kundi la wafanyakazi ndilo linalofaidika zaidi.

Akitoa maoni yake katika mada iliyotolewa na katibu wa MRENGO iliyochambua katiba iliyopo na wajibu wa kila raia kujitokeza kuchangia, Allan Mkopoka, mkulima Alfani Awezaye, alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wakulima kujitokeza siku hiyo na kueleza yote ambayo kwao ni kikwazo.

“Nchi yetu ni ya wakulima na wafanyakazi lakini wenzetu wanafaidika zaidi na rasilimali za nchi kuliko sisi na ukiangalia sisi ndio wengi ambao tunazalisha zaidi….wenzetu wanalipwa pensheni, bima ya matibabu, sisi tunapotaka huduma hizo tunaambiwa tuchangie, hivi wanataka tuchangie mara ngapi…usawa upo wapi?”, alihoji  Aawezaye.

Omari Alfani na Mzee Chipojola, walitaka katika ijayo itamke wazi kuwa mkulima atapewa fidia na serikali iwapo msimu husika utakumbwa na ukame kutokana na mabadiliko ya tabianchi au athari nyingine za kimazingira ikiwa ni pamoja na mafuriko.

“Tangu utoto wako umechangia nchi hadi unazeeka kupitia kilimo, leohujiweni kwanini serikali isikulipe kiinua mgongo, kwanini bei ya mazao inaposhuka serikali isitufidie… inapotokea tumeshindwa kuvuna kutokana na hali ya hewa kubadilika serikali pia inapaswa kutufidia”, alisema Chipojola.

Awali akifungua mdahalo huo katibu tawala wa wilaya hiyo,Beatus Bitegeko, alisema kuwa ni wajibu kwa kila mwananchi kujitokeza mara tume hiyo itakapofika ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kutoa maoni na kuwezesha kuwa na katiba itakayomgusa kila mtu kwa namana moja au nyingine.

“Nataka nitoe wito kwenu mliopo hapa na wengine walio majumbani, mara tume itakapofika hapa wilayani jitokezeni kuchangia msiache wachangie wachache alafu baadae mjilaumu au kuiona katika itakayotungwa haina manufaa kwenu”  alisema Bitegeko.

Mwisho.

 

 

 

 

 

Advertisements